Viongozi wa vyama vya siasa Tarafa ya Buguruni, wametakiwa kudumisha amani katika kipindi cha kampeni na wakati wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa, unatarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Buguruni Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Thedius Kaihuzi katika ukumbi wa kituo cha Polisi Buguruni alipokuwa akizungumza na Viongozi wa vyama vya siasa.
Amesema, “niwaombe sana Viongozi wangu tushirikiane kuimarisha usalama katika Mitaa yetu kwa kufanya kampeni zilizo safi na ambazo hazitapelekea kutokea kwa jinai.”
Kaihuzi pia aliwataka Viongozi hao kufuata sheria na kanuni zilizowekwa na Mamlaka husika zinazosimamia uchaguzi kwa kuhakikisha wanatoa elimu kwa wafuasi wao ili kuepuka kuingia katika jinai zisizo za lazima kwa kuhakikisha wanafuata misingi bora ya kampeni kwa kutumia lugha rafiki kwa Wagombea wakati wa kampeni.
Kwa upande wake Katibu Mwenezi wa Chama cha Mapinduzi – CCM Wilaya ya Ilala, Geofrey Lawi alilishukuru Jeshi la Polisi kwa elimu aliyowapatia na kuahidi kuzingatia misingi yote kama ambavyo sheria ilivyoelekeza.
Alisema, “naomba tukutoe wasiwasi Afande OCD, sisi Viongozi wa vyama vya siasa tunaahidi kuwa mabarozi wazuri kwa wafuasi wetu na tunakuhakikishia kipindi cha kampeni sambamba na zoezi la uchaguzi kwa ujumla litakamilika kwa usalama kabisa.”
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo – CHADEMA, Manase Mjema ameliomba Jeshi la Polisi kuendelea kutoa elimu mara kwa mara kwa vyama vya siasa na kwa askari kwa ujumla ili kila upande uweze kushirikiana katima kuimarisha amani na usalama katika kipindi cha uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 hadi uchaguzi Mkuu kwa mwaka 2025.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Viongozi wa vyama vya siasa wapatao 40 kutoka vyama mbalimbali ikiwemo Chama cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), CUF, ACT Wazalendo na Chama cha Makini.