Mahakama ya Wilaya ya Kwimba Mkoani Mwanza imemhukumu kifungo cha miaka 30 jela Kulwa Nkingwa (30) mkazi wa Sumve kwa jina maarufu Maduka, kwa kosa la kumbaka mtoto wa miaka 11.
Hukumu hiyo imetolewa Novemba 19, 2024 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo Ndeko Dastan Ndeko, baada ya upande wa Jamhuri kutoa ushahidi mbele ya Mahakama hiyo pasipo kuacha shaka kwamba mshtakiwa ametenda kosa hilo.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, mshtakiwa alitenda kosa hilo Mei 6, 2024 nyumbani kwa Mganga wa Jadi aitwaye Aloyce John huko katika Kijiji cha Sumve, ambako mtoto huyo alikuwa amepelekwa kutibiwa.
Mshtakiwa alifikishwa katika Mahakama hiyo Julai 02, 2024 na kusomewa shtaka la kubaka na Mwendesha Mashtaka wa Serikali Juma Kiparo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo Ndeko Dastan Ndeko, kinyume na kifungu cha 130 (1) (e) na kifungu cha 130 (1) vya Kanuni ya Adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2022.
Nkingwa ametiwa hatiani katika kesi hiyo ya jinai namba 12898 ya mwaka 2024. Aidha, baada ya kusomewa hukumu mwendesha Mashtaka Juma Kiparo aliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa kwani kosa hilo linahusisha ukatili wa kijinsia kwa kuwa binti huyo ni mdogo sana na kitendo hicho kimemuathiri kisaikolojia.