Faudhia Simba, Dar24 Media – Dar es Salaam.
Ni bora ukose vyote kwenye maisha lakini sio furaha, kwani uzuri wa maisha unachagizwa na furaha kutokana na wengi kufurahia vile wavipendavyo na mojawapo ya furaha hizo inatoka kwenye mchezo wa Soka ambao umebeba furaha ya watu wengi Duniani ikiwemo Tanzania.
Na kiuhalisia furaha huwa inapatikana pale ambapo Mtu amepata kile anachokipenda na alichokuwa na hamu nacho, tukiamini kwamba Watu wengi wanataka kuishi maisha maisha marefu na ya furaha, au walau kuepuka maisha mafupi na mabaya ambayo huleta makasiriko nafsini.
Lakini changamoto huja pale ambapo unataka kugeuza uelewa huu wa furaha kuwa ushauri na tiba ambavyo inaweza kumnufaisha mtu na kurefusha maisha ya kiafya kulingana na inavyofikiriwa kisayansi ikiwemo raha yaMpira ambayo wengi imewasababishia furaha ama masikitiko.
Sote tunatambua kwamba fFraha ya mpira haielezeki, kupitia mpira unaweza kushusha thamani ya mtu na kuipandisha pia sababu ya sababu ya kushinda ama kushindwa, au kama ilivyo sasa hapa nchini ambapo Watanzania karibu wote wana furaha baada ya Timu yao ya Taifa Stars kufuzu michuano ya AFCON.
Ushindi huu, umewafanya Stars waondoke kifua mbele huku nao wakiamini kwamba Watanzania wote wameshinda, kwani mchango wao kama mashabiki umechagiza matokeo chanya kwa kuujaza uwanja kisha kushangilia bila kupoa hadi pale walipohitimisha ushindi wao wa 1-0 dhidi ya Taifa la Guinea katika mchezo wa kundi H uliochezwa Novemba 19, 2024 Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.
Mfungaji wa bao la Tanzania alikuwa ni Mshambuliaji wa Al Talaba ya Iraq, Simon Msuva dakika ya 61 ya mchezo huo akimalizia pasi ya kiungo wa Klabu ya Yanga, Mudathir Yahy Abbas, ushindi ambao uliifanya Taifa Stars kufikisha poini 10 baada ya kucheza mechi sita na kuungana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) yenye pointi 12.
Ni mara ya nne katika historia ya Tanzania kufuzu AFCON baada ya mwaka 1980 nchini Nigeria, 2019 Misri, 2023 Ivory Coast na hii pia inakuwa ni mara ya kwanza kufuzu fainali mbili mfululizo na kumfanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwapatia zawadi ya Milioni 700 kama pongezi.
Kumbe inawezekana, sasa wapi huwa tunafeli na kuwatelekeza Wachezaji kuipambania nchi peke yao na matokeo yanapokuwa mabaya lawama zinaenda kwa Wachezaji zikitolewa sababu mbalimbali kwamba Wachezaji husika hawakustahili kuitwa, Kocha mbovu, Stars bado sana kiasi tunawakatisha tamaa na wao kukosa morali.
Si mnamkumbuka hadithi ya Kinjekitile Ngwale? aliweza kuwapa ujasiri Wanajeshi yake akisema maji yatageuka kuwa risasi japo kiuhalisia haikuwa hivyo lakini bidii zake ziliteta upinzani wa kutosha kiasi kwamba heshima ilikuwepo, sisi mbinu kama hizi tunazishindwaje tena katika wakati kama huu wenye kila kitu.
Hamasa kubwa kama hizi za mashabiki kujaza uwanja huwa tunazikosa sana, matokeo yake tunawategemea wahamasishaji kama akina Bongo Zozo, Wasemaji wa Vilabu, Manara na wengine ambao nguvu yao ndani ya uwanja haiwezi kufua dafu, hamasa zinatakiwa ziende mbali zaidi kwa kila mtu kuchukua nafasi yake ili kupata matokeo chanya.
Tuondoe Usimba na Uyanga unaotuletea makundi kwenye jambo la nchi, kwani mtindo huo unadhohofisha jitihada mfano hata inapotokea Wachezaji wameitwa basi Wahusika huanza kukosoa kuona mchezaji fulani wao wanaomuamini pale anapokuwa hayupo hii si sawa.
Ni ngumu kupigana na adui anayekufahamu vizuri, uadui wa Stars unaanzia nyumbani kwa kukosa sapoti ya wachezaji wa jukwaani ambao ni Mashabiki wa Taifa ambao wametuonesha nguvu yao ya mchezaji wa 12 uwanjani kiasi Guinea ilipelekewa ‘moto’ na ushindi tukaupata kisha shangwe likatawala pale Lupaso.
Ndugu zangu Hamasa njema ni siri ya mafanikio ambayo nayo huleta furaha maishani, hebu tuwe na uwezo wa kufanya jambo likafanikiwa naamini tukiamua tunaweza nadhani mfano mmeuona kwa macho na hata masikio yalisikia, licha ya kuwa tulikuwa na msiba wa wenzetu walioangukiwa na jengo pale Kariakoo, lakini tuliweza kushikamana tukashinda.
Sote tunahusika kwa namna fulani katika‘sanaa ya uhamasishaji, kutia moyo na kushawishi wengine katika mwelekeo fulani kama ilivyojidhihirisha majuzi na kutokana na mtazamo huo inatuonesha kwamba kila mtu ni mhamasishaji, lakini ikiwa hamasa itakuja kwa mtindo wa agizo, basi huwa ni muhimu sana kuifanikisha (TUMEFANIKISHA).
Hata hivyo, huduma ya uhamasishaji ina mwelekeo mwingine muhimu na tofauti, ikibeba ufahamu na ubora wa wito wa mtu binafsi, ikikumbukwa kwamba Mhamasishaji huwa ana msukumo wa kiroho wa ndani, wajibu na shauku ya kutia moyo wengine kufanikisha jambo fulani, hakika Wtanzania ni wahamasishaji bora sana. (TUMESHUHUDIA)