Mbunge wa Vijana Mkoa wa Ruvuma (CCM) ambaye pia ni Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga anaendelea na kazi ya kuhamasisha Wananchi katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Ruvuma ili waweze kujitokeza kwa wingi kupiga kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 27 mwaka huu.

Baada ya ziara ya mafanikio aliyoifanya wilayani Namtumbo, Kapinga amefanya ziara pia wilayani Mbinga kwa kuanza na Vijiji vya Mkako na Kigonsera ambapo amewaasa Wananchi kuchagua Viongozi bora watakaosimamia shughuli za maendeleo katika Mitaa, Vijiji na Vitongoji hapa nchini.

“Wananchi mliopo katika Kata ya Kigonsera, Mkako na maeneo yote ya Mbinga ifikapo Novemba 27, 2024 jitokezeni kushiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa ili mchague Viongozi makini kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM),” amesisitiza Kapinga.

Amesema lazima umakini uwepo katika uchaguzi wa Viongozi kwani ndio watakuwa wasimamizi wakuu wa miradi ya maendeleo kwenye maeneo ya Wananchi hivyo waangaliwe watu watakaoweza kuongoza wananchi kwa ufanisi pamoja na miradi ya maendeleo.

Pamoja na kuhamasisha Wananchi kushiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Kapinga ametoa wito kwa wadau mbalimbali wa maendeleo ngazi ya Taifa hadi Kitongoji kushirikiana na Serikali katika kuwafikishia wananchi maendeleo na huduma bora ikiwemo afya, elimu n.k

Picha: Rais Samia akitunukiwa Shahada ya Udaktari wa Heshima
Uchaguzi: Wana CCM msipuuzie upigaji kura - Suzan