Mfumo wa Usimamizi wa Ununuzi wa Umma Kielektroniki, unaojulikana kama NeST, umefanikiwa kufika kwenye fainali za Mashindano ya Tuzo ya Ubunifu wa Mifumo, na kuwa miongoni mwa mifumo mitano bora barani Afrika.

Mashindano hayo yanayoratibiwa na African Association for Public Administration and Management (AAPAM) chini ya uangalizi wa Umoja wa Afrika (AU), yanaendelea jijini Kampala, Uganda.

Timu ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), ikiongozwa na Mkurugenzi Mkuu, Dennis Simba, ilifanya wasilisho lake mbele ya jopo la majaji wa kitaalamu kutoka nchi mbalimbali za Afrika, Novemba 25, 2024 jijini humo.

Akiwasilisha, Simba alieleza jinsi Mfumo wa NeST, uliojengwa na wataalam wa Tanzania, ulivyokuwa suluhisho muhimu kwa changamoto nyingi zilizokuwepo katika ununuzi wa umma barani Afrika, na hasa nchini Tanzania. Alisisitiza kuwa, kupitia mfumo huu, Serikali ya Tanzania imeweza kuokoa kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 4.95 (USD 4.95 milioni) kutokana na kukomesha matumizi ya karatasi na toner.

“Hadi Oktoba 2024, zaidi ya wazabuni 25,000 wamejisajili kwenye mfumo, na zaidi ya Mashirika 30,000 ya Ununuzi yanatumia NeST kuboresha michakato ya ununuzi na kuhakikisha wanazingatia sheria na kanuni. Watumiaji waliosajiliwa wameunda akaunti 41,300, na programu ya NeST kwa simu imepakuliwa na zaidi ya watu 30,000, ikiwa na alama ya nyota 4.3 kwa urahisi wa matumizi,” alisema Simba.

Baada ya wasilisho hilo la takribani dakika 45, Bw. Simba, akiwa na Mkurugenzi wa Mifumo ya TEHAMA wa PPRA, Michael Moshiro, na Mtaalam wa Ununuzi, Dkt. Magoti Harun, alisisitiza kuwa mafanikio haya ni matokeo ya maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye aliagiza Serikali ijikite katika matumizi ya teknolojia kutatua changamoto za ununuzi wa umma.

Fainali za mashindano hayo zitafanyika Novemba 28, 2024, jijini Kampala, mbele ya mamia ya wadau kutoka nchi mbalimbali barani Afrika na mshindi atatangazwa siku hiyo. Jopo la majaji limefanya utafiti wa kutosha kabla ya kuingia kwenye usaili wa uwasilishaji.

Byabato, Godson wauwasha moto hitimisho la Kampeni Kagera
Sendiga azindua huduma za awali Jengo la Mama, Mtoto Oltotoi