Boniface Gideon, Handeni – Tanga.

Chama cha The National League For Democracy (NLD) leo kimefunga kampeni zake za majukwaani mkoani Tanga Tarafa ya Misima Wilayani Handeni mkoani Tanga kwa kulia na kero ya maji katika maeneo mbalimbali nchini, ambapo Wilayani  humo dumu moja la Maji likipanda kwa kuuzwa Sh.1000 kutoka Sh.500 bei ya awali.

Katibu Mkuu wa NLD Taifa, Doyo Hassan Doyo akizungumza na mamia ya Wakazi wa Tarafa hiyo kwenye viwanja vya soko la Misima alisema kero ya maji Wilayani humo imefikia hatua mbaya hali iliyosababisha maji kupanda bei.

“Kero hii ya maji Wilayani Handeni na maeneo mengine Nchini ni ya muda mrefu sana,inatumika kisiasa kwaajili ya kuombea kura,sisi NLD tukiingia madarakani tutahakikisha tunachukua hatua za vitendo ili kuwapunguzia Wananchi mzigo mkubwa wa maisha, kwenye Wilaya hii ya Handeni,”

“dumu Moja la maji ni Sh.1000 ili familia ipate maji kwa siku moja, walau wapate madumu 5, kwahiyo ukizidisha mara siku 30 ni Sh.150,000 bado hawajala na kuvaa na matumizi mengine, Wakazi hawa hawana vipato vikubwa, maisha ni magumu kwao mana mlo mmoja kwa siku, tunawaomba Wananchi muwachague viongozi ambao watajali shida zenu na kuzitatua,” alisisitiza Doyo.

Doyo aliongeza kuwa chama kimejipanga kuwasaidia Wananchi nakwamba endapo wagombea wake watachaguliwa jambo kubwa watakaloanza nalo ni kuwasimamia watendaji wa Serikali kutatua kero sugu kwenye jamii ikiwemo maji,ajira na migogoro ya Ardhi.

Amesema, “NLD imejipanga kuhakikisha inawatulia Wananchi kero zao,kero zipo nyingi sana kwenye jamii yetu, kiukweli zinahitajika juhudi binafsi,waliokuwepo madarakani wameshindwa kuwasaidia Wananchi, walitanguliza maslahi yao binafsi, tumeliona hilo na ndio mana tumewasimamisha wagombea wasiokuwa na njaa,wagombea wetu wote wanauwezo wakutoa ajira kwa wengine kupitia fursa walizonazo na wengi wao wametoa ajira kwenye jamii inayowazunguka.”

Kwa upande wake Mwenyekitiwa Chama hicho Wilaya ya Handeni, Rajabu Doyo aliitaka Takukuru kufanya uchunguzi haraka iwezekanavyo kwa baadhi ya wagombea na vyama vya siasa kuandika Barua za kujitoa kwenye Uchaguzi wa Serikali za mitaa.

“Haiwezekani mgombea alichukua fomu ya kugombea akaijaza alafu akairudisha , alafu leo unaambiwa kajitoa ,hii ni rushwa ya wazi wazi kabisa, kwahiyo tunaomba TAKUKURU iliangalie hili iingilie kati haraka iwezekanavyo,” alisisitiza Rajab.

TANZIA: Lala salama Dkt. Faustine Ndugulile
Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Novemba 27, 2024