Swaum Katambo, Mpimbwe – Katavi.
Jumla ya wagonjwa 403 wamefanyiwa vipimo vya Macho katika Halmashauri ya Mpimbwe Jimbo la Kavuu Mkoani Katavi, ambapo kati yao wagonjwa 140 walikutwa na tatizo la mtoto wa jicho.
Vipimo hivyo, vilifanywa na timu ya utabibu wa magonjwa ya macho kutoka Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Katavi na Hospitali ya Wilaya ya Mpimbwe walioendesha kliniki ya afya ya macho Wilayani humo, kwa majuma mawili.
Akitoa thamini ya zoezi hilo, Mratibu wa Afya ya Macho Mkoa wa Katavi, Dkt. Salome Renatus amesema wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na wagonjwa wengi waliojitokeza kupona kabisa, ambapo huduma hiyo pia ilihusisha upasuaji kwa baadhi ya wagojwa.
“Watu wengi waliojitokeza wameweza kupona kabisa na kurudi katika hali ya kawaida wapo ambao tumewafanyia huduma ya upasuaji hii ni kutokana na macho yao kuhitaji matibabu ya kina,” amesema Dkt. Salome.
Aidha, amemshukuru Mbunge wa Jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Geophrey Pinda kwa kuwapa ushirikiano hasa kuwahamasisha Wananchi kufika hospitalini hapo.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo hilo Geophrey Pinda amesema kufanyika kwa huduma ni kuunga jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan hasa kuboresha miundombinu ya afya.
Naye Mzee Antony Lutonja (78), amesema amehangaika kwa miaka mitatu kutafuta tiba ya macho ambapo hatimaye timu hiyo imempa matumaini mapya ya kupona kutokana na huduma hiyo.
Amesema, “sijaona huduma kama hii kwingine yaani nilale leo niamke naona kama wengine mambo yanafanyika hapa ni mambo mazuri mno.”
Huduma hiyo ya macho ipo chini ya ufadhili wa Shirika la Afya kutoka Ujerumani la African Blind help.