Swaum Katambo – Katavi.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geophrey Pinda amewataka wenyeviti wa vijiji na vitongoji nchini kuacha kuuza ardhi za wananchi kinyemela ili kuzuia migogoro ya ardhi.

Pinda ameyasema hayo katika hafla ya kuwaapisha wenyeviti wa vijiji na vitongoji wa serikali za mitaa iliyofanyika katika ukumbi wa shule ya Sekondari Usevya iliyopo Halmashauri ya Mpimbwe mkoani Katavi.

“Mwenyekiti hakai ofisini, anatembea na kafaili kameandikwa ardhi, hamuonyeshi hata mtendaji wake wa kijiji, yaani anatembea na mihuri kwenye kibegi hiyo hapana..,na maeneo mengi watu wengi wamekosa uenyekiti kwa sababu ya dhuluma kwenye ardhi,” amesema

Ameongeza kuwa mwenyekiti hana mamlaka peke yake ya kuidhinisha mauzo ya eneo isipokuwa kwa kushirikiana na halmashauri.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko amesema migogoro mingi ya ardhi imekuwa ikisababishwa na wenyeviti wa mitaa na vitongoji wasio waadilifu kwa kuwalaghai wananchi ikiwemo kugushi nyaraka za mauzo ya ardhi.

Aidha Mrindoko amewataka wenyeviti hao kufanya kazi kwa hofu ya Mungu katika kipindi chao chote cha utumishi wao katika nafasi zao.

Kwa upande wake Mjumbe wa NEC Taifa Gilbert Sampa amewataka wenyeviti hao waliochaguliwa kwenda kusimamia Ilani na kuwaletea maendeleo wananchi.

Wenyeviti wote walioapishwa katika hafla wametoka Chama Cha Mapinduzi CCM huku wenyeviti wa vitongoji 654 sawa na 98.8% pia wameshinda nafasi hizo kupitia CCM.

Rais Samia akutana na Wakuu wa Nchi EAC