Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema ataunda Tume mbili ambapo moja itachunguza na kutoa mapendekezo kuhusu masuala ya ardhi yanayolalamikiwa na wakazi.
Taarufa iliyotolewa kwa vyombo vya Habari na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Sharifa Nyanga hii leo Desemba Mosi, 2024 imeeleza kuwa, Tume nyingine itaangalia utekelezaji wa zoezi zima la uhamiaji kwa hiari kutoka eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.
Rais Dkt. Samia ameyasema hayo leo Ikulu ndogo ya Arusha wakati akizungumza na viongozi wa kimila wa jamii ya Kimaasai (Malaigwanani) wanaoishi katika eneo la Ngorogoro.
Mkutano huo umefanyika kwa lengo la kuwasikiliza viongozi hao kufuatia kuwepo kwa malalamiko dhidi ya baadhi ya maamuzi ya Serikali yanayohusu eneo la Ngorongoro.
Rais Dkt. Samia amewahakikishia kuwa Serikali itaendelea kuimarisha utendaji kazi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) kwa lengo la kuimarisha mahusiano kati ya Serikali na jamii hiyo.
Aidha, taarifa hiyo ilpia imeeleza kwamba Rais Samia amesisitiza ulazima wa Wananchi kushirikishwa ipasavyo katika upangaji na utekelezaji miradi inayopita kwenye maeneo yao.
Amebainisha kuwa, Tanzania ni nchi inayojivunia umoja wa kitaifa na yenye Serikali inayowahudumia Watanzania wote. Hivyo, ameitaka Ofisi ya Rais TAMISEMI kushughulikia changamoto zinazojitokeza ikiwemo kukosekana kwa baadhi ya huduma za msingi za kijamii katika eneo la Ngorongoro.