Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri amezindua Kampeni ya Nipendezeshe Nisome inayolenga kusaidia vifaa vya shule kwa watoto wenye mahitaji maalumu ,ambapo watoto zaidi ya 500 wanatarajiwa kufikiwa.
Akizungumza leo Desemba 4, 2024 jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo Shekimweri amesema, pamoja na serikali kuwekeza kwenye sekta ya elimu, bado wapo baadhi ya watoto kwenye kaya masikini ambao wanashindwa kwenda shule kutokana na kukosa vifaa vya shule.
Amesema kutokana na hali hiyo ipo haja kwa jamii kujenga utamaduni wa kusaidia wenye uhitaji ili waweze kupata haki yao ya msingi ya kusoma.
Mwenyekiti wa Kampeni hiyo inayoratibiwa na Redio moja ya jijini Dodoma, Sonatah Nduka amesema kampeni hiyo imelenga kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalum vifaa vya shule ikiwemo sare,madaftari, chakula pamoja na vitabu.
Amesema, “kupitia Kampeni tunalenga kuwafikia watoto wenye uhitaji katika mwaka 2024/2025 watoto zaidi ya 500 kuwapatia vifaa ili waweze kusoma kama ilivyo kwa watoto wengine.”
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule Msingi Dodoma Makulu, Amon Sebyiga amesema watoto 30 katika Shule yake watanufaika kampeni hiyo.