Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Sinde Warioba ameonya hatua ya Jeshi la Polisi kuingizwa kwenye siasa, akisema limekuwa likitoa matamko ambayo yatawagawa Wananchi huku akisisitiza kuwa hatua hiyo ina madhara.

Jaji Warioba ameyasema hayo hii leo Desemba 4, 2024 wakati alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam huku pia akisisitiza Jeshi la Ulinzi nalo lisije likaingizwa kwenye mambo ya siasa.

Amesema, “katika miaka michache iliyopita tumeliingiza Jeshi la Polisi kwenye siasa, linatoa matamko ya kisiasa na hii italeta mgawanyiko. Wananchi watagawanyika. Kuna wale watakaoona, Jeshi la Polisi ni adui, tusifike huko. Tuliache Jeshi la Polisi lifanye kazi zake za kawaida.”

Warioba ameongeza kuwa, ‘kwa bahati nzuri Rais (Samia Suluhu Hassan) alipoingia madarakani alisikia malalamiko ya wananchi kuhusu suala hilo na kuunda Tume ya Haki Jinai.”

“Tume ikaleta mapendekezo mazuri na ikapendekeza, Jeshi la Polisi liachwe lifanye kazi zake, lakini sasa hivi tumeliingiza Jeshi la Polisi kwenye siasa, lakini ujue polisi wale ni raia wa kawaida, ikifika kwenye mambo ya siasa wana mawazo yao, wakienda kupiga kura kila mmoja ana mapenzi yake,” alifafanua Jaji Warioba.

REA kusambaza Mitungi ya Gesi ya kilo sita Tabora
Kampeni nipendezeshe nisome kuwanufaisha Watoto 500 Dodoma