Afarah suleiman, Simanjiro – Manyara.
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mwl.Fakii Raphael Lulandala, Desemba 4, 2024 amefunga mafunzo ya Jeshi la Akiba (Mgambo) katika kata ya Oljoro namba tano, Wilayani humo.
Akiwa katika hafla hiyo ya kufunga mafunzo, Lulandala ametoa wito na kuwataka wahitimu hao kutotumia mafunzo yao kama chachu ya kufanyia vitendo vya uhalifu kama kuonea watu, kuwinda wanyama pori na matendo yote ya kiarifu bali watumie mafunzo hayo kama sehemu ya kuleta Amani katika jamii inayowazunguka.
“Niwapongeze kwa kushiriki mafunzo haya ambayo yamewapatieni stadi muhimu moja ukakamavu mbili kuwafanya ninyi kuwa walinzi wenu nyie wenyewe binafsi lakini pia jamii yetu na nchi kwa ujumla,”
“hivyo kuwafanya kuwa na sifa ya kuwa Askari wa Jeshi la Akiba na kuanzia leo majukumu yale mnayopaswa kuyafanya kama Askari mtaruhusiwa kuyafanya pasina kukiuka sheria,” amesema Lulandala.
Katika hafla hiyo Lulandala ametoa maelekezo kwenye kamati ya ulinzi na Usalama ya wilaya Simanjiro endapo patatokea nafasi zozote zinazohitaji askari ama ambapo Askari wakiwa hawatoshelezi basi ni vyema kuwatumia Vijana hao wa Jeshi la Akiba.
Jumla ya wahitimu thelathini Wanaume 27 na Wanawake watatu walipatiwa mafunzo hayo.