Takriban Wabunge 16 na Maafisa wengine watatu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamenusurika kifo kufuatia ajali iliyohusisha basi la Kampuni ya Shabiby aina ya Yutong lenye namba za usajili T 149 EGM na Lori la mizigo aina ya Scajua namba T 941 ARJ likiwa na Tela namba T 153 ARY.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, George Katabazi amesema ajali hiyo imetokea eneo la Mbande Wilayani Kongwa Barabara kuu ya Dodoma kuelekea Morogoro.
Amesema, “Dereva (Bahati Saidy Juma (42), tunamshikilia kwa sababu yeye ndio chanzo cha ajali hiyo,” huku ikidaiwa kuwa majeruhi walikimbizwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma General wengine Hospitali ya Uhuru na baadhi katika Hospitali ya Benjamim Mkapa zote za Mkoani Dodoma.
Wabunge hao walikuwa wakisafiri kuelekea Jijini Nairobi Nchini Kenya kwenye Mashindano ya michezo ya Mabunge ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.