Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Nishati limekutana jijini Arusha kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali yanayohusu Wafanyakazi wa Wizara husika.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt.Khatibu Kazungu amefungua Mkutano wa Baraza hilo jijini Arusha, Desemba 6, 2024 na kueleza kuwa kufanyika kwa Mkutano huo ni utekelezaji wa sheria mbalimbali zinazoelekeza waajiri wote kuhakikisha wanaunda mabaraza ya wafanyakazi mahala pa kazi.

“Kufanyika kwa mikutano hii ya Mabaraza ya Wafanyakazi kunatokana na agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la mwaka 1970, Sheria ya Utumishi wa Umma sura na.298 ya mwaka 2002 na kanuni zake za mwaka 2022 ikisomwa kwa pamoja na sheria ya majadiliano kazini ya mwaka 2004 pamoja na sheria ya ajira na mahusiano kazini ya mwaka 2004.” Amesema Dkt. Kazungu.

Ameeleza kuwa, Mkutano huo wa Sita wa Baraza la Wafanyakazi utakuwa na majukumu mbalimbali ikiwemo kupokea taarifa ya utekelezaji wa Bajeti ya Wizara kwa mwaka 2024/25 kuanzia mwezi Julai-Desemba 2024, utekelezaji wa majukumu ya Wizara kwa mwaka 2024 (Julai-Desemba) na kupitia Mpango wa Mafunzo wa Wizara wa mwaka 2024/25-2026/27.

Ameongeza kuwa, katika Baraza hilo pia itatolewa taarifa kuhusu kiasi cha fedha kilichopitishwa na Bunge kwa mwaka 2024/2025, fedha zilizopokelewa, majukumu yaliyotekelezwa, changamoto zilizojitokeza na mbinu zilizotumika kutatua changamoto hizo ili kuweza kusonga mbele kwa mafanikio na ufanisi zaidi.

Amesema kuwa kwa mwaka 2024/2025 fedha iliyoidhinishwa na Bunge kwa Wizara ni sh trilioni 1.8 huku sh. trilioni 1.7 ikiwa ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo na matumizi ya kawaida yakiwa ni sh.bilioni 88.8.

Dkt. Kazungu amesema kuwa, Wizara ya Nishati imeendelea kuhakikisha kwamba bajeti inazingatia stahiki za kisheria za watumishi kama vile malipo ya nauli za likizo na posho ya kujikimu.

Kwa upande wake, Meshack Lugeiyamu kutoka TUGHE Taifa ameipongeza Menejimenti ya Wizara ya Nishati kwa kuwa na ushirikiano chanya na Wafanyakazi wa Wizara ambao amesema kuwa kwa kiasi kikubwa unaimarishwa na vikao vinavyofanyika mara kwa mara kati ya pande hizo mbili ambavyo ni sehemu ya kupata mrejesho wa masuala mbalimbali kuhusu watumishi.

Vilevile amesema Wizara ya Nishati ni ya kuigwa mfano kutokana na kufanya mikutano ya Baraza la Wafanyakazi kwa mujibu wa taratibu na kalenda.

Katika Mkutano huo wa sita wa Baraza la Wafanyakazi Wizara ya Nishati, ametambuliswha Mwenyekiti Mpya wa TUGHE Tawi la Nishati ambaye ni Zuena Msuya.

Kaulimbiu ya Mkutano huo ni Matumizi ya Nishati ya Safi ya Kupikia kwa Maendeleo Endelevu ya Tanzania.

Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Desemba 7, 2024
Wabunge wanusurika katika ajali ya Basi, Lori Dodoma