Hii leo Desemba 9, 2024 Tanzania inasherehekea maadhimisho ya miaka 63 ya Uhuru ambayo hufanyika kila mwaka ikiakisi kumalizika kwa utawala wa kikoloni wa Muingereza.
Katika siku hii mwaka 1961, Tanzania wakati huo ikiitwa Tanganyika ilipata uhuru kutoka kwa Uingereza ambapo siku hiyo, Desemba 9, kulikuwa na furaha kama ilivyo sasa.
Sherehe rasmi zilifanyika Uwanja wa Taifa na wakati huo huo kulikuwa na Mwenge wa Uhuru uliopelekwa kwenye kilele cha mlima Kilimanjaro.
Kwa heshima ya mafanikio haya ya kihistoria, Serikali kiuhalisia huwa inafuatilia sekta zake kwa kutaja mafanikio yake, matatizo na changamoto ilizozikabili tangu ipate Uhuru na kupanga mwelekeo wa baadaye.
Tanganyika ambayo mwaka mmoja baada ya Uhuru ilitangazwa kuwa Jamhuri, ilijiunga na iliyokuwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar mwaka 1964 kuunda taifa jipya la Tanzania.
Hii leo sherehe ambazo kwa kawaida hupamba maadhimisho ya siku ya Uhuru zimefutwa, baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuelekeza fedha zilizotengwa kwa ajili ya dhifa na maonesho, zielekezwe katika kutoa huduma za kijamii.
Uamuzi kama huo wa kuzifuta sherehe za uhuru uliwahi pia kuchukuliwa mwaka 2015 na baadae mwaka 2020 chini ya utawala wa Rais wa awamu ya tano hayati John Pombe Magufuli.
Rais Samia anataka kila mkoa uhakikishe Wilaya zake zinafanya shughuli za kijamii ikiwemo upandaji miti, usafi wa mazingira katika maeneo ya kijamii kama vile kwenye Masoko, Hospitali, Kambi za wazee na wenye mahitaji maalum.
Aidha, ameelekeza pia mashindano ya michezo mbalimbali pamoja na makongamano na midahalo ya kujadili maendeleo endelevu ambayo nchi imefikia katika kipindi cha miaka 63 ya Uhuru.
Mapema, Serikali ilitoa wito kwa Wananchi kushiriki katika shughuli hizi ili kujivunia sifa za kipekee ambazo zimetokana na Uhuru Kauli Mbiu ya Maadhimisho hayo ikiwa ni Miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara: “UONGOZI MADHUBUTI NA USHIRIKISHWAJI WA WANANCHI NI MSINGI WA MAENDELEO YETU.”
Hata hivyo, sote tunakumbuka kwamba Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ndiye alidai uhuru wa Tanganyika na ndipo Desemba 1961, ilishushwa bendera ya Uingereza na kupanda Bendera ya Tanganyika na ndipo Mwalimu Nyerere akawa Waziri wa Kwanza.
Aprili 26, 1964 Tanganyika na Zanzibar ziliungana kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hapo kiongozi wa Tanganyika Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipata kuwa Rais wa kwanza (1964-1985) na kiongozi wa mapinduzi ya Zanzibar Abedi Amani Karume akawa Makamu wa Kwanza wa Rais.
Tanzania, chini ya Rais wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi (1985-1995), iliruhusu mfumo wa vyama vingi vya siasa Tanzania na kuanza mpango wa kurekebisha uchumi kuendana na masharti ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani.
Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa (1995-2005) aliendeleza mfumo wa uchumi wa soko huria ambapo mashirika ya umma yanabinafsishwa.
Desemba 21, 2005 Jakaya Kikwete aliapishwa kuwa Rais wa nne (2005-2015), naye aliendeleza sera za watangulizi wake kwa kauli mbiu ya Maisha bora kwa kila Mtanzania.
Aliyemfuata mwaka 2015 ni rais wa tano John Pombe Magufuli aliyerudia awamu ya Pili 2020, lakini kwa mapenzi ya Mungu naye ametangulia mbele ya haki na ambaye Watazania wanaendelea kukumbuka yote hasa urithi mkubwa na sifa ya uchapakazi aliyoiacha.
Na Rais wa awamu ya sita ni Samia Suluhu Hassani, yeye anasema Kazi iendelee kutokana na baadhi ya mafanikio ya Tanzania kwa kipindi cha miaka 63, ikiwemo kuulinda uhuru na mipaka, amani, kuimiraisha uchumi, kuboresha huduma za kijamii, kuimarisha demokrasia nk.