Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, limefanikiwa kupunguza matukio ya ukatili wa kijinsia kutoka matukio 1,140 mwaka 2023 hadi 1,118 kwa mwaka 2024 sawa na upungufu wa asilimia 22.
Hayo yamebainishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Naibu Kamishna wa Polisi, Wilbrod Mutafugwa wakati wa Maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia yaliyofanyika kimkoa katika uwanja wa Polisi Mabatini jijini humo.
Amesema, kupungua kwa matukio hayo kumetokana na jitihada zinazofanywa na Jeshi la Polisi kupitia Mtandao wa Polisi wanawake (TPF NET), Dawati la Jinsia na Watoto na Polisi Kata wa kutoa elimu na kuchukua hatua za kisheria kwa watuhumiwa wa masuala ya ukatili.
Maadhimisho hayo huadhimishwa kila mwaka nchini ifikapo Novemba 25 hadi Disemba 10 ikiambatana na siku ya haki za binadamu.
Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia ziliasisiwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) awamu ya 7 Kofi Annan mwaka 2006 kwa lengo la kutaka dunia itambue kuwa lipo tatizo kubwa la ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto ulimwenguni.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi ambaye alikuwa mgeni rasmi katika Maadhimisho hayo ameitaka jamii kupaza sauti kwa pamoja kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Sambamba na hayo wadau mbalimbali waliohudhuria Maadhimisho hayo wametaja baadhi ya sababu zinazosababisha uwepo wa ukatili wa kijinsia ikiwemo afya ya akili na kuliomba Jeshi la Polisi kuendelea kukemea na kuchukua hatua za kisheria kwa watuhumiwa wa vitendo hivyo.

TANESCO tunathamini Wadau wa Maendeleo - Mha. Nyamo-Hanga
Mapigano: Basi lashambuliwa, 22 wauawa