Leo Tanzania imeandika historia nyingine katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya umeme baada ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko kuzindua utekelezaji wa mradi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma  na upanuzi  wa vituo vya kupoza umeme vya  kilovoti 400 Chalinze-Pwani na Zuzu-Dodoma.

Mradi huo wa umeme uliozinduliwa utawezesha umeme wote unaozalishwa katika mradi wa kuzalisha umeme wa JNHPP kufika katika maeneo yote ya mikoa iliyopo Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Ziwa, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Kati, Kanda ya Magharibi, Migodi, Viwanda na kuimarisha biashara ya umeme Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Dkt. Biteko amesema kutekelezwa kwa mradi huo kunatokana na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuendelea kutoa fedha za kutekeleza miradi mbalimbali pamoja na miongozo yake ya namna bora ya kutekeleza miradi ili kuhakikisha nchi inakuwa na umeme wa uhakika kwa lengo la kukidhi mahitaji ambayo yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku kutokana na ukuaji wa shughuli za kiuchumi na kijamii.

Amesema kuwa kutokana na jitihada hizo zinazofanywa na Rais Samia katika kuendeleza miradi ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji umeme imepelekea Tanzania kuwa kinara barani Afrika katika usambazaji wa umeme kwa wananchi na hii ni kutokana na takwimu zilizotolewa na Benki ya Dunia.

Ameeleza kuwa, Serikali imeendelea na jitihada za kuimarisha upatikanaji wa nishati ya umeme nchini ambazo zimewezesha kuongeza uwezo wa mitambo ya kufua umeme iliyopo nchini hadi kufikia Megawati 3,169.26 ambapo mahitaji ya juu ya umeme nchini kwa sasa yamefikia Megawati 1,888.72 ambapo mahitaji hayo hayajawahi kufikiwa kutoka nchi ipate Uhuru na hii ikimaanisha kuwa uchumi unazidi kukua kutokana na kuongezeka kwa shughuli za maedeleo.

“Kuimarika kwa uzalishaji wa umeme nchini kumechangiwa na  kuanza uzalishaji katika Mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) wenye uwezo wa kuzalisha Megawati 2,115 ambao hadi sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 99.6 na jumla ya Megawati 1,175 za umeme zinazalishwa na kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa,“ amesema Dkt. Biteko.

Katika Hafla hiyo, Dkt. Biteko amekemea vikali wahujumu wa miundombinu ya umeme ambao amesema kuwa wanarudisha nyuma uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika kuwafikishia wananchi nishati ya uhakika na kuagiza Vyombo vya Ulinzi na Usalama kuchukua hatua kali kwa wahujumu hao ambao oia wamekuwa wakikosesha wananchi umeme pale miyndombinu inapoharibiwa.

Kuhusu Wakandarasi wa mradi huo, Kampuni ya TBEA kutoka China, amewataka wahakikishe mradi  unakamilika kwa wakati ili wananchi wapate manufaa yaliyokusudiwa ikiwa pia ni maelekezo ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Dkt. Biteko ametumia hafla hiyo kuwakumbusha viongozi na wananchi kuhusu jitihada za Serikali katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kutimiza lengo la Serikali la asilimia 80 ya Watanzania  kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.

Katika muendelezo wa jitihada hizo, amesema Serikali imetoa ruzuku kwa mitungi ya gesi zaidi ya 400,000 itakayouzwa kwa nusu gharama ya bei ya soko ambapo mitungi hiyo inasambazwa katika Mikoa yote Tanzania Bara.

Ametoa wito kwa Watanzania kutumia nishati safi ya kupikia kwa kutumia majiko ya gesi na teknolojia mbalimbali kulingana na mazingira ikiwemo nishati ya umeme kwani nishati hizi ni miongoni mwa nishati safi, salama na ya gharama nafuu ikilinganishwa na matumizi ya kuni na mkaa.

Vilevile ametoa wito kwa wadau mbalimbali na wafanyabiashara nchini kuhakikisha majiko yanayotumia nishati fanisi ya umeme yanapatikana kwa wingi na kwa bei nafuu ili wananchi wengi katika maeneo mbalimbali wakiwemo wa vijijini waweze kutumia umeme kwa ajili ya kupikia.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa ameipongeza Wizara ya Nishati na TANESCO kwa uzinduzi wa mradi huo wa usafirishaji umeme na upanuzi wa vituo vya kupoza umeme vya  Zuzu Dodoma na Chalinze na kueleza kuwa utekelezaji wa mradi huo unaakisi dhamira ya Rais Dkt. Samia ya kutaka watanzania wapate nishati ya uhakika.

Bashungwa amesema kuwa Serikali inatoa fedha nyingi ili kutekeleza miundombinu ya umeme hivyo Wizara yake itahakikisha miundombinu hiyo inalindwa kwa wivu mkubwa na kuwashughulikia wahalifu wa moundombinu hiyo,

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amempongeza Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanyika katika Sekta ya Nishati na pia amempongeza Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko kwa kusimamia Sekta kwa weledi, ufanisi, uzalendo na uchapakazi wa hali ya juu.

Amesema mradi uliozinduliwa leo ni muhimu kwani Tanzania inategemewa kuimarisha hali ya umeme kwa nchi za Mashariki mwa Afrika kupitia miradi ya uzalishaji na usafirishaji umeme ambayo inaendelea kufanyika.

Amesema moja ya masuala yaliyokuwa yakitiliwa mkazo katika Mkutano uliohusu biashara ya kuuziana umeme na kununua umeme kwa nchi Wanchama Mashariki mwa Afrika (EAPP) ni uunganishaji umeme kati ya Tanzania na Kenya ambapo leo laini hiyo ya umeme ya kV 400 imewashwa na pongezi zimetolewa kwa Rais Samia na Dkt.Biteko kwa kutekeleza mradi huo.

Kwa upande wake, Katibu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema sasa nchi inazalisha zaidi ya megawati 3000 za umeme na hii inaifanya Tanzania kuwa nchi inayozalisha umeme mwingi kuliko nchi zote za Afrika Mashariki na hivyo kutoa fursa kwa Tanzania kufanya biashara ya umeme na nchi nyingine za Afrika iikwemo Burundi, Rwanda, Uganda na Kenya.

Amesema mradi huu utaenda katika kanda mbalimbali ikiwemo mikoa ya Kaskazini na kuingia hadi nchini Kenya.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga alisema mradi wa kusafirisha umeme kutoka Chalinze hadi Dodoma umegawanyika katika sehemu kuu mbili ambazo ni  ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme katika msongo wa kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma yenye urefu wa kilomita 345 na upanuzi wa vituo vya kupokea na kupoza Umeme vya Chalinze (400/220/132kV) mkoani Pwani na Zuzu (400/220/33kV) Mkoani Dodoma.

Alisema  malengo ya mradi huo ni kuwezesha usafirishaji wa umeme wote (2,115MW) utakaozalishwa katika Bwawa la JNHPP na kuufikisha kwenye maeneo yote ya mahitaji ya umeme, hatua itakayosaidia kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme kwenye Gridi ya Taifa na kuongeza uwezo wa kusafirisha umeme kwenda mikoa yenye viwanda na migodi ya uchimbaji madini ya Kaskazini Magharibi, Kaskazini Mashariki, Kanda ya Kati na Kusini mwa Tanzania.

Alieleza kuwa, lengo lingine la mradi ni kuwezesha zoezi la uunganishaji umeme kwa pamoja katika mifumo ya Mashariki mwa Afrika (Eastern Africa Power Pool – EAPP) na Kusini mwa Afrika (Southern Africa Power Pool – SAPP) na hivyo kuwezesha kufanyika kwa biashara ya nishati ya umeme kikanda (Regional Power Trading).

Aliongeza kuwa, Mradi husika unagharamiwa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 100 kwa jumla ya gharama ya Shilingi 513 Bilioni ambapo Mkandarasi  Kampuni ya TBEA kutoka China  ameshalipwa malipo ya awali ya kiasi cha Shilingi bilioni 107.93 ambayo ni asilimia 20 ya gharama za mradi.

Alieleza kuwa katika mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme, kazi mbalimbali zimeanza na mradi utakamilika mwaka 2026 mwezi Septemba huku mradi wa upanuzi wa vituo vya kupoza umeme kazi pia zinaendelea na mradi utakamilika Septemba 2026.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge amesema mradi huo ni uthibitisho wa kazi kubwa na nzuri za Dkt. Samia Suluhu Hassan na kwamba umeme huo utafaidisja Tanzania na nchi nyingine za Afrika na ni sehemu pia ya uhamasishaji wa nishati safi ya kupikia kwani wananchi watatumia umeme huo kupikia.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima amesema wananchi mkoani Morogoro wanatambua  kazi kubwa iliyofanywa na Rais Samia katika kuendeleza miradi ya umeme ikiwemo kukamilisha miradi ya miaka mingi ukiwemo wa kuunganisha umeme kati ya Tanzania na Kenya.

Mwakilishi wa Wadau wa Maendeleo katika hafla hiyo, Wendy Hughes ambaye ni Mkurugenzi wa Benki ya Dunia  Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kujikita katika kuiimarisha gridi ya taifa ya umeme ambayo ni muhimu katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii pamoja na kutoa uhakika wa usalama wa nishati.

Amesema kuwapo kwa mifumo imara ya usafirishaji umeme itafanya wananchi kufikishiwa umeme wa uhakika katika maeneo mbalimbali ya nchi na pia   ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa kufikisha umeme kwa watu milioni 300 barani Afrika ifikapo 2030.

Ameahidi kuwa Wadau wa Maendeleo wataendelea kutoa  ushirikiano kwa Tanzania ili kukamilisha mipango mbalimbali ya maendeleo ambayo nchi imejiwekea.

Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Desemba 12, 2024
M-Bet, HaloPesa kuwazawadia mashabiki wa soka kupitia Kampeni ya Amsha Amsha