Timu ya Serikali ya Majadiliano ya Mradi wa Kuchakata na Kusindika gesi asilia (LNG) imeendelea na ziara yake nchini Indonesia ya kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu utakelezaji wa miradi ya LNG.

Timu hiyo inayoongozwa na Naibu Katibu Mkuu Nishati – Mafuta na Gesi, Dkt. James Mataragio imekutana na Rais na Mtendaji Mkuu wa kampuni ya PERTAMINA ya nchini Indonesia, Simon Aloyslus Montiri pamoja na viongozi waandamizi wa kampuni hiyo, ambapo walijadili fursa za uwekezaji katika sekta ya nishati ikiwepo mkondo wa juu wa petroli, nishati mbadala, uzalishaji wa mbolea pamoja na sekta nyingine za kiuchumi.

Kwa hapa nchini, kampuni ya PERTAMINA inamiliki hisa nyingi za kampuni ya Maurel et Prom ambayo inafanya shughuli za uendelezaji na uzalishaji wa gesi asilia katika kitalu cha Mnazi Bay kilichopo mkoani Mtwara.

Aidha, Montiri amefarijika kukutana na timu hiyo ya Majadiliano ya Tanzania na ameahidi kushirikiana na Wizara ya Nishati na Taasisi zilizochini yake katika kuhakikisha rasilimali ya gesi iliyogundulika hapa nchini inazalishwa kwa manufaa ya nchi na watanzania kwa ujumla.

Baada ya kikao hicho, timu hiyo ya Majadiliano ya LNG itaendelea na ziara yake kwa kutembelea mitambo ya kuzalisha LNG nchini Indonesia kwa ajili ya kujifunza juu ya uendeshaji wa miradi ya hiyo.

Ashikiliwa na Polisi kwa kukata Nyeti za mumewe
Maisha: Kamali yamlaza Polisi Eliudi