Johansen Buberwa – Kagera.
Waajiri wa Watumishi wa Umma wametakiwa kuwaruhusu wafanyakazi wao pale wanapohitiji kujiendeleza na masomo, ili waweze kuongeza ufanisi wa utendaji kazi kwa kuleta tija katika maeneo ya uzalishaji kiuchumi.
Wito huo, umetolewa na Mkuu wa Mkoa Kagera Hajjat Fatma Mwasa katika Mahafali nane ya Chuo Kikuu Huria Tawi la Kagera, ambapo amesema Wafanyakazi wanapotoa ombi kusoma kwa waajiri wao, lipokelewe kwa manufaa ya taasisi hizo.
Amesema, “mimi niwaombe sana Waajiri mlioko Mkoa wa Kagera elimu haina mwisho na elimu ni ufunguo wa maarifa wafanyakazi wenu wanapo omba kusoma tupokee kwamba ni jambo chanya na ni kwa manufaa ya Taasisi zetu,”
“Ninaamini kwenye bajeti zetu tunaweka mipango ya watu kusoma kwa hiyo tusifanye choyo tutoe ruhusa wakasome na pale tunapoweza kuwasaidia malipo tuwasaidie wakasome faida ya elimu yao itarudi kuja kuleta tija katika shughuli wanazozifanya kwenye Taasisi.”
Katika hatua nyingine, Hajjat Mwasa amesema atashirikiana na uongozi wa chuo hicho kupata wahisani kwa ajili ya kukarabati baadhi ya majengo yaliyochaka, ili kuwepo na muonekono mzuri wa kuvutia pamoja na kuwapatia Kompyuta tano.
Awali akisoma Risala ya Wahitimu, Frabius Ngemera amesema kwa sasa wanakabiliwa na upungufu wa viti ambavyo huleta changamoto wakati wa Mitihani na tatizo sugu la kutopata ruhusa kwa Waajiri wao wakati wa Masomo, Mitihani na shughuli mbalimbali za Vyuo kwani asilimia kubwa ya wanaosoma elimu ya juu ni Watumishi wa umma.
Naye Mkuu wa chuo hicho, Medard Rembesha amesema kwasasa wameleta elimu kwa njia ya masafa ya mtandaoni, ambayo Mwanafunzi shahada ya kwanza ya mpaka miaka sita anaweza kusoma kwa miaka mitatu, njia ambayo humpatia fursa na nafasi.