Klabu ya Manchester United imeendelea kufanya vyema chini ya Kocha Ruben Amorim baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya mahasimu wao Manchester City. Katika mchezo huo Manchester City walikuwa wa kwanza kupata bao la uongozi kupitia kwa Josko Gvardol dakika ya 36 ya mchezo na City kwenda mapumziko wakiwa kifua mbele.
Kipindi cha pili dakika ya 85 ya Mchezo Amad Dialo wa Manchester United aliangushwa ndani ya Box la 18 na kupelekea penati iliyofungwa na Bruno Fernandez. Dakika ya 90 Amad Dialo alirejea tena langoni mwa City na kuandika bao la pili akimalizia pasi ya Laurato Martinez.
Ushindi huu unamfanya Kocha Amorim kuendelea kuwa na rekodi nzuri ndani ya klabu hiyo baada ya kushinda michezo 4 sare 1 na kupoteza michezo miwili.
Guardiola akalia kuti kavu
Kocha wa Manchester City Pep Guardiola ameendelea kufanya vibaya ndani ya kikosi hicho akipoteza michezo 8 kati ya 10 na sare 2. Huu ni mwendelezo mbaya kwa mabingwa hao watetezi wa EPL. Kikosi cha City kimekuwa kikipitia changamoto nyingi kwa siku za hivi karibuni kutokana na majeraha ya baadhi ya wachezaji lakini pia migogoro ya nje ya uwanja imekuwa ikivuruga mwenendo wa timu.
Kwa sasa kikosi cha Guardiola kinashikilia nafasi ya 5 kikiwa na alama 27 katika michezo 16 waliyocheza. Huu ni mwendelezo mbaya zaidi kwa kocha huyo aliyejiungha miaka 10 iliyopita klabuni hapo.