Naibu Waziri, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulika afya, Dkt. Festo Dugange amesema lengo la serikali ni kuona namna gani Halmashauri zinaendelea kujenga uwezo wa kukusanya mapato ya ndani na kukamilisha miradi mbalimbali ya kuwahudumia wananchi kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri husika.
Dkt. Dugange ameyasema hayo katika kongamano la wadau wa Serikali za Mitaa ili kujadili namna ya kuhamasisha utawala bora na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi lililoandaliwa na Tasisi ya Uongozi kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI lililofanyika Jijini Dodoma.
“lengo la serikali ni kuona namna mamlaka zetu zinaendelea kujenga uwezo wake wa kukusanya mapato ya ndani ndio maana kila wakati tuna sisitiza kila Halmashauri kubuni vyanzo vipya vya mapato na kuvisimamia kwa ufanisi unaotakiwa,” aliongeza Dkt. Dugange.
Amesema, ni lazima kusimamia na kukusanya mapato kwa ufanisi kwenye vyanzo vya mapato ambavyo vimekwisha kuibuliwa na vimeanza kuzalisha ili viwe na tija kwa Mamlaka husika kwani kumekuwa na changamoto kubwa katika ukusanyaji wa mapato ikiwemo matumizi ya fedha mbichi, fedha kutokwenda benki na fedha kutumika tofauti na mipango husika.
Aidha, Dkt. Dugange amesema Serikali itaendelea kusimamia swala la utawala bora, kukuza demokrasia, kuimarisha ushirikishwaji wa wananchi na kuchochea ugatuaji wa madalaka kwa Umma ili kuongeza ukuaji wa Uchumi shindani, kuongeza ukusanyaji wa mapato na kudhibiti matumizi katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa.