Mahakama ya Uingereza, imewahukumu vifungo vya maisha baba na mama wa kambo wa mtoto Sara Sharif (10), raia wa Uingereza mwenye asili ya Kipakistani, aliyekufa baada ya kuteswa kwa muda mrefu.

Baba huyo Urfan Sharif (43), amehukumiwa kifungo cha miaka 40, huku mkewe Beinash Batool (30), akihukumiwa kifungo cha miaka 33 kwa mauaji hayo.

Waliohukumiwa kwa kifo cha Mtoto Sarah ni Urfan Sharif (kushoto), Beinash Batool (katikati) na Faisal Malik (kulia).

Mbele ya Mahakama, Jaji John Cavanagh alieleza kuwa mwili wa Sarah ulipatikana ukiwa na majeraha makubwa akiwa amevunjika baadhi ya viungo pamoja na kuwa na majeraha ya kuchomwa na pasi.

Amesema, Mtoto Sarah alikuwa muathirika wa mateso ya kupitiliza na kwamba Sharif na Batool hawakuonesha dalili zozote za kujutia matendo yao na alikutwa akiwa amekufa kitandani mwake mwezi Agosti 2023 akiwa peke yake nyumbani.

Mtoto Sara Sharif (10) enzi za uhai wake.

Aidha, uchunguzi wa maiti ulionesha kuwa Sara alikuwa na majeraha 71 na kuvunjika mifupa mara 25, huku mjomba wake, Faisal Malik (29), pia akipatikana na hatia ya kusaidia au kuruhusu mauaji hayo na kuhukumiwa kifungo cha miaka 16.

Magereza Unguja, Pemba kuanza matumizi Nishati safi ya kupikia
Ajali ya Lori, Coaster yauwa 14 Morogoro