Mkazi wa kitongoji cha Mwankuba, kijiji cha Nyambiti, Wilaya ya Kwimba, mkoani Mwanza, Mashauri Ng’oga Shauri (20) amehukumiwa kifungo cha maisha baada ya kukutwa na hatia ya kumlawiti mtoto wa miaka minne ambaye jina tunalihifadhi kwa sababu za kisheria, mkazi wa kijiji cha Nyambiti ambaye ni ndugu wa mshtakiwa ambaye ni mtoto wa baba yake mdogo.

Hukumu hiyo imesomwa Desemba 17, 2024 katika shauri la jinai namba 31963 la mwaka 2024 na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Kwimba, John Jagadi mbele ya mwendesha mashtaka wa Serikali Juma Kiparo.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka kama ilivyosomwa na Mwendelezo maashtaka wa Serikali, Juma Kiparo mshtakiwa alitenda kosa hilo Oktoba 27, 2024 katika kijiji cha Nyambiti, kilichopo wilaya ya Kwimba na mkoa wa Mwanza kinyume na kifungu cha 154(1) (a) na (2) cha Kanuni ya Adhabu sura namba 16 ya sheria marejeo ya mwaka 2022.

Mtuhumiwa alifikishwa mahakamani Novemba 11, 2024 na kusomewa shitaka la kulawiti na siku hiyo hiyo mwendesha mashtaka aliiomba Mahakama hiyo isikilize mashahidi wawili akiwemo mhanga pamoja na mzazi wake baada kusomewa hoja za awali.

Baada ya kusikiliza mashahidi wanne wa Jamhuri, Hakimu Jagadi amejiridhisha kwamba ushahidi uliotolewa dhidi ya mshtakiwa ni mzito na kwamba upande wa mashtaka umethibitisha Shauri hilo pasi na kuacha Shaka.

Mshtakiwa alipopewa nafasi ya kujitetea kwa nini asipewe adhabu kali na aliiomba Mahakama hiyo imuachie huru kwa kuwa ni mkosaji wa mara ya kwanza kitendo kilichopingwa na mwendesha mashtaka aliyeiomba Mahakama kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa kwa sababu kitendo hicho ni cha kinyama na cha ukatili uliopitiliza.

Aidha, aliikumbusha Mahakama kujielekeza kwenye kifungu kidogo cha pili cha kifungu cha 154 cha Kanuni ya Adhabu ambacho kinaelekeza kwamba mtuhumiwa endapo atafanya kosa hilo kwa mtoto mwenye umri chini ya miaka 18 akipatikana na hatia anapaswa kuhukumiwa jela kifungo cha maisha.

Jagadi alisema licha ya shufaa za mshtakiwa kuomba kupunguziwa adhabu lakini kifungu kilichotajwa na mwendesha mashtaka kinamfunga mikono na hivyo hana adhabu mbadala bali ni kumhukumu.

Uzembe Sekta ya ununuzi waweza hujumu miradi ya Serikali - Simba
Maisha: Skudu sasa kapona, ni Mwanaume kamili