Utafiti mpya umefichua kwamba uvutaji sigara wa mapema hasa ngazi ya utoto huongeza hatari ya kukumbwa na maradhi ya moyo maishani.
Utafiti huo pia umeonesha kuwa watoto wengi wanaoanza matumizi ya Tumbaku katika umri wa miaka 10 au katika umri wa balehe, huendelea na tabia hiyo hata baada ya kufikisha miaka 20.
Utafiti huo, umehusisha ushirikiano kati ya chuo kikuu vya Bristol na Exeter, nchini Uingereza na Chuo Kikuu cha Eastern Finland, ulichapishwa kwenye jarida la the Journal of the American College of Cardiology (JACC).
Watafiti wametoa takwimu hizo baada ya kuwafuatilia Watoto 1,931 waliozaliwa miaka ya tisini kuanzia walipokuwa na umri wa miaka 10 hadi walipofika miaka 24.
Takriban thuluthi tatu ya wale walioanza kuvuta sigara utotoni au katika umri wa kubalehe, waliendelea hadi mwanzoni mwa utu uzima.
Matumizi ya kila mara ya tumbaku kuanzia umri wa miaka 10 kuendelea hadi miaka 24, yalihusishwa na asilimia 52 ya visa vya uharibifu wa moyo mapema maishani, ambapo matatizo haya yalikuwa pamoja na moyo kuvimba, moyo kupunguza uwezo wa kujilegeza, na shinikizo la damu, kufikia miaka 24.
Tafiti za awali kwa watu wakomavu zimeonyesha kwamba uvutaji sigara kuanzia umri wa kubalehe, huongeza hatari ya maradhi ya moyo kufikia umri wa makamo.
Hata hivyo, hakuna utafiti wa awali ambao ulichanganua ishara za mapema za uvutaji tumbaku kuanzia utotoni, kwa moyo.
“Ni hatari sana kuanza kuvuta sigara katika umri huu mdogo, huku visa vya ongezeko la idadi ya vijana walio katika umri wa kubalehe wanaovuta sigara za kieletroniki.
Bidhaa za sigara hizi huwa na viungo hatari kwa mapafu, na pia husababisha hitilafu kwenye mapigo ya moyo, hali ambayo yaweza kusababisha uharibifu wa kiungo hiki.
Wanaotumia sigara za kieletroniki pia bila kujua wanajiweka hatarini,” alisema Andrew Agbaje, Profesa mMshiriki toka Chuo Kikuu cha Eastern Finland.
“Utafiti huu unaonyesha kwamba mbali na kusababisha hatari ya kukumbwa na maradhi ya moyo baadaye maishani, uvutaji sigara katika umri wa kubalehe, hupelekea uharibifu wa kudumu kwenye misuli ya moyo,” alisema Emily Bucholz, Profesa msaidizi katika Kitivo cha udaktari cha Chuo Kikuu cha Colorado School of Medicine.
crediT@TaifaLeo