Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ameagiza Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha miradi ya dharura iliyo chini yake.

Waziri Ulega ametoa maagizo hayo kwenye mkutano wake na Menejimenti na Mameneja wa TANROADS wa mikoa yote nchini uliofanyika mjini Dodoma ambapo aliwaambia miradi ya dharula inapaswa kushughulikiwa kidharura.

Amesema, “fanyeni kazi kwa kasi tena usiku na mchana hususan kwenye miradi ya dharura ili kuwawezesha Watanzania kuondokana na adha ya miundombinu iliyoharibiwa.”

ATAKA KASI YA KIJESHI MIRADI YA DHARURA

Katika hatua nyingine, Waziri Ulega pia  amewataka mameneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) kuogeza spidi katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa barabara.

Amewaambia mameneja hao kuwa wanatakiwa waende kwa spidi inayofanana na viwango vya kasi vinavyoonekana wakati Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) linapopewa majukumu ya utekelezaji na serikali kwa sababu kuna mvua zinakuja na zinaweza kufanya maeneo yaliyoharibika kuharibika zaidi.

Ulega amesema barabara zilizoharibika kwa sababu ya mvua za masika zilizochanganyika na zile za El Nino zimesababisha usumbufu na kusimamisha shughuli za uchumi na hivyo ni muhimu zikashughulikiwa kwa haraka.

Ijuka Omuka: Dkt. Biteko ataka uwekezaji zaidi Kagera
Kilimo kilivyobeba maana kubwa, mifumo mbalimbali