Madereva wa Pikipiki za magurudumu mawili maarufu kama Bodaboda wa Kijiji cha Shamwengo kilichopo Kata ya Inyala Halmashauri ya Mbeya Vijijini, wametakiwa kushirikiana na Jeshi la Polisi na uongozi wa Kijiji kuimarisha ulinzi.
Rai hiyo, imetolewa na Polisi Kata ya Inyala Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Charles Kyogolo alipotembelea Kijiji hicho na kukutana na madereva Bodaboda wa Kijiji cha Shamwengo.
Mkaguzi Msaidizi Kyogolo amewataka kujitokeza kuongeza nguvu katika vikundi vya ulinzi shirikishi vinavyofanya kazi ya kuimarisha ulinzi kupitia doria za usiku zenye lengo la kuwabaini wahalifu na kuzuia uhalifu katika Kijiji hicho.
Aidha, amewakumbusha la utoaji wa taarifa za uhalifu na wahalifu na kuwataka kutoficha taarifa wala wahalifu kwani Jeshi la Polisi kupitia wao litahakikisha linachukua hatua kwa mujibu wa sheria kwa yeyote atakayekuinika kujihusisha na uhalifu au kula njama.
Pia, amewataka madereva hao kujiepusha kuendesha chombo cha moto wakiwa wamelewa pombe, kuacha kupakia abiria zaidi ya mmoja, kuendesha chombo cha moto bila kuwa na leseni hai ya udereva.