Mwenyekiti wa chama cha Demokrasia na Maendeleo – CHADEMA, Freeman Mbowe amesema atagombea Uenyekiti wa chama hicho, nafasi ambayo amekuwa akihudumu kwa takriban miaka 20 sasa.
Mbowe ametoa tamko hilo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na Vyombo vya Habari hii leo Desemba 21, 2024 ikiwa ni baada ya kuwaomba wanachama na baadhi ya viongozi wa CHADEMA kumpa saa 48 ili kuamua ikiwa atagombea nafasi hiyo.
Amesema, “Nimetafakari kwa kina sana, nimesema mara nyingi nilitamani kuondoka lakini siwezi kuondoka na minyukano ambayo ipo ndani ya Chama , kwahiyo CHADEMA nipo, nitakuwepo, nitagombea na Mimi na Viongozi wenzangu wanaoniunga mkono na wasioniunga mkono naamini tutakutana kwenye mazungumzo tuweke mambo sawa, sijawahi kuzuia Watu kugombea, anayetaka kugombea tukutane kwenye box.”
Mbowe ameongeza kuwa, “Wazee walioasisi Chama chetu hawakuondoka madarakani kwakuwa walitaka kung’atuka, waliamua kuondoka kwasababu walikuwa wametimiza wajibu wao mkubwa wa kujenga Chama imara chenye itikadi na sera madhubuti.
“Tukumbuke Mzee Edwin Mtei Mwenyekiti wa kwanza wa Chama aliondoka akiwa na umri wa miaka 68, miaka mitano baadaye Mzee Bob Makani Mwenyekiti wa pili yeye aliondoka akiwa na miaka 67, wote waliondoka sio kwasababu ya kushindwa bali kwakuwa walikuwa wamemaliza kazi zao za kuimarisha sera,” alifafanua zaidi Mbowe.