James Mwanamyoto OR-TAMISEMI.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Serikali itajenga shule, zahanati, sekondari na kituo cha afya ili kusogeza huduma za kijamii kwenye makazi mapya ya waathirika wa maporomoko ya tope Hanang mkoani Manyara.

Majaliwa amesema hayo akiwa Wilayani Hanang, wakati akikabidhi nyumba 109 kwa waathirika wa maporomoko ya tope wilayani humo, ambazo zimejengwa na Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Msalaba Mwekundu kwenye Kitogoji cha Waret kijiji cha Gidagamowd.

Amesema, “tunataka wananchi hawa wawe na mwingiliano na wengine,waendelee kuishi hapa na wapate huduma muhimu za kijamii na ndio maana tutajenga shule, zahanati, sekondari na kituo cha afya.”

Majaliwa amefafanua kuwa, kati ya nyumba hizo 109 alizozikabidhi kwa waathirika wa maporomoko ya tope, nyumba 73 zimegharamiwa na Serikali, nyumba 35 zimegharamiwa na Shirika la Msalaba Mwekundu Tanzania na nyumba moja imegharamiwa na Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT).

Ameongeza kuwa, nyumba zote hizo zimejengwa kwa uratibu mzuri wa timu ya wataalam kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Fedha, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Hanang pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Hanang.

Majaliwa pia ameipongeza na kuishukuru TARURA kwa ujenzi mzuri wa barabara kwenye eneo hilo ambalo zimejengwa nyumba 109 za waathirika wa maporomoko ya tope na kuongeza kuwa toka amefika na kuanza ukaguzi wa nyumba hajaona barabara iliyoteleza licha uwepo wa mvua iliyokuwa ikinyesha.

“Mhe. Waziri wa TAMISEMI na TARURA yako mmefanya kazi nzuri sana ya ujenzi wa barabara kwenye nyumba hizi 109, hivyo jukumu mlilobakia nalo ni kutuwekea lami hivyo jaribu kuangalia kwenye vifungu vyako vya bajeti ili barabara ziwekwe lami,” alisema Majaliwa.

Maporomoko ya tope wilayani Hanang yaliyotokea Desemba 7, 2023 katika mji mdogo wa Katesh pamoja na vijiji jirani yalipelekea baadhi ya wakazi wa maeneo hayo kupoteza nyumba za kuishi.

Baadaye, Serikali ilichukua hatua ya kukabiliana na changamoto hiyo na hatimaye Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa amekabidhi nyumba 109 kwa waathirika wa maporomoko hayo.

Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Desemba 22, 2024
Nitagombea Uenyekiti CHADEMA - Mbowe