Jeshi la Polisi Nchini, kupitia kwa Mkuu wake IGP Camillus Wambura limefanya mabadiliko madogo kwa Wakuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani kwa kumhamisha Naibu Kamishna wa Polisi, Ramadhani Ng’anzi kutoka Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania kwenda Makao Makuu ya Upelelezi Dodoma kuwa Mkuu wa Kitengo cha Makosa ya Maadili ya Jamii.
Taarifa ya Jeshi hilo iliyotolewa hii leo Desemba 22, 2024 imeeleza kuwa, nafasi ya Ng’azi imechukuliwa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, William Mkonda ambaye alikuwa Mkuu wa Usalama Barabarani Kanda Maalum ya Dar es Salaam.
Aidha, IGP pia amemhamisha aliyekuwa Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi wa Polisi, Boniphace Mbao kwenda kuwa Mkuu wa Usalama Barabarani Kanda Maalum ya Dar es Salaam.
Aliyekuwa Mkuu wa Elimu kwa Umma Kikosi cha Usalama Barabarani Nchini, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Michael Deleli amehamishiwa Makao Makuu ya Polisi Dodoma, kuwa Kaimu Mkuu wa Maadhimisho ya Kitaifa.
Taarifa hiyo imebainisha kuwa, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Nassoro Sisiwaya aliyekuwa Mkuu wa Operesheni Kikosi cha Usalama Barabarani Nchini, yeye amehamishiwa Mkoa wa Kilimanjaro kwenda kuwa Mkuu wa Usalama Barabarani.