Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limesema linachunguza taarifa ya kifo cha mwanafunzi mmoja wa chuo Kikuu cha Dodoma – UDOM, ambaye alifariki kwa maji.

Taarifa ya Kamanda w Polisi Mkoani humo, Alex Mkama imeeleza kuwa tukio hilo limetokea Desemba 22, 2024 majira ya mchana huko kwenye maporomoko ya maji Sanje yaliyopo katika hifadhi ya taifa ya Udzungwa, Kata ya Sanje, Wilaya ya Kilombero Mkoa wa Morogoro.

“Hezekiel Petro (21), Mwanafunzi wa mwaka wa kwanza chuo kikuu cha Dodoma masomo ya sanaa na historia alikufa kwa maji baada ya kukanyaga jiwe au mwamba wenye utelezi na kutumbukia kwenye maji yenye kina kirefu,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha, Mwanafunzi huyo inadaiwa alifika hapo akiwa kwenye ziara ya mafunzo kwa vitendo na Wanafunzi wenzake zaidi ya 300 wakiwa wamefuatana na wakufunzi wao.

Mwili wa Mwanafunzi huyo uliweza kutolewa kwenye maji na wataalamu wa kuogelea na taratibu zingine za uchunguzi zinaendelea.

Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi limetoa wito kwa Wananchi wote kuchukua tahadhari na kufuata maelekezo ya wataalamu wanapotembelea maeneo yenye upekee.

Msaada kwa Taiwan: Marekani inacheza na Moto - China