Afarah Suleiman, Babati – Manyara. 

Mkoa wa Manyara umepanga kuandikisha Watoto 66,135 wa Elimu ya awali ambao wanategemewa kuanza shule Januari 13, 2025 sawa na asilimia 40 ya walioandikishwa huku watoto wa darasa la kwanza wakitarajiwa kuwa 59,987 sawa na asilimia 65 ambapo zoezi la uandikishwaji likiwa bado linaendelea.

Mipango ya Serikali katika sekta ya Elimu kwa mwaka 2025 ni kwamba watoto wote wenye sifa ya kuanza shule wapelekwe mashuleni kwakua kumekuwa na ongezeko la shule mpya za msingi 38 ambapo za Sekondari zikiwa 17 huku pia maboresho ya miundombinu kwenye Sekta hiyo yanaendelea.

Serikali pia imefanya jitihada kwa wanafunzi waliofaulu darasa la Saba Kwa mwaka 2024 ambao ni 28,804 wote wamepangiwa kwenda kuanza Shule kidato Cha kwanza ifikapo 13 January 2025.

Hayo yamezungumzwa na Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga wakati akizungumza na waandishi wa Habari ofisini kwake kuhusu mambo mbalimbali ikiwemo maendeo yaliyopatikana ndani ya Mkoa huo hasa Sekta ya Elimu na kueleza mipango ya Serikali kwa mwaka 2025.

Amesema ongezeko la shule hizo ni nyingi na zinaendelea kuongezeka kila wakati kulingana na uhitaji wa eneo husika lengo ni kuhakikisha kwamba watoto wote walioandikishwa kwenda shule wanakwenda shule.

“Nyongeza hii ya majengo kuongezeka na ukarabati wa madarasa ,madawati,matundu ya vyoo inaonyesha ni kwa namna gani serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya sekta ya elimu nchini kukidhi matakwa na matarajio ya wazazi na walezi ya kuwapatia elimu watoto wao”. Sendiga amesema

“Asilimia mia moja ya watoto wenye ufaulu wa darasa la saba mkoani humo wamepangiwa kujiunga na shule za sekondari wamepangiwa shule na wataripoti tarehe 13 Januari 2025 bila kukosa”

Amesema,moja ya jitihada za Serikali ni ongezeko la shule za msingi na sekondari ambapo katika majengo ya shule za msingi ndipo pia huwekwa na watoto wa shule ya awali.

Kuhusiana na suala la uwepo wa chakula mashuleni Mkuu wa Mkoa Sendiga àmetoa maelekezo kwa Maafisa Elimu kuwashirikisha wazazi kuona namna Bora ya utoaji wa chakula utafanyika ili Kila mzazi aweze kuwajibika ipasavyo na kulibeba jukumu hilo.

Aidha,katika msimu huu wa sikukuu Sendiga amewaasa wazazi na walezi kuwalinda watoto wao wasifanyiwe vitendo vya kikatili ikiwa pamoja na kuwaangalia mienendo Yao ya kitabia na kuwarekebisha.

Ameongeza Kwa kusema kuwa Serikali inatoa Elimu bure hivyo mzazi hapaswi kuchangia chochote Zaidi ya kusimamia majukumu yanayompasa kwa kuhakikisha anapata mahitaji yake muhimu ikiwemo kununua Sare za Shule.

Mkuu wa Mkoa Queen Sendiga amewashukuru wananchi wa Mkoa huo kwa kutoa ushirikiano na Serikali na kusema kuwa mafanikio yaliyopatikana yametokana na wao hivyo amewaomba kuendelea kutoa ushirikiano kwa mwaka 2025 kwa lengo la kujenga Taifa.

Same: Sita wafariki kwa Mvua, mazao yaharibiwa
Polisi waanza uchunguzi kifo cha Mwanafunzi wa UDOM