Hakuna sheria katika Mataifa mengi ya Ulimwengu yanayoruhusu au kuadhibu rasmi Wachawi, lakini kiutendaji “wazee hao busara” hupewa nafasi ya ushauri au maamuzi ndani ya baadhi ya jamii, ili kubaini kama kuna mtu ni “mchawi” au kurekebisha matukio kadhaa ya kiimani au kimila pale yanapoenda kombo.

Utaratibu huu ndiyo umepelekea kutokea kwa msiba mzito katika Taifa la Angola, baada ya kuandaliwa mchakato wa kuwafanya wale wanaoitwa “wachawi” kunywa kinywaji cha mitishamba kiitwacho “Mbulungo” wakiamini kwamba mtu akifa watu wanaojihusisha na tiba za kienyeji wakinywa Mbulungo na wakidhurika, huaminika kwamba wanajihusisha na uchawi.

Machi 13, 2024 Msemaji wa Polisi wa Mkoa wa Camacupa, António Hossi Samba alitangaza kwenye Redio ya Taifa kuhusu tukio la Watu zaidi ya hamsini wanaoshutumiwa kwa “uchawi” kufariki baada ya kulazimishwa kunywa mchanganyiko wa mitishamba, ili kubaini kama wanafanya vitendo vya uchawi na kuonya juu ya ongezeko la hivi karibuni la kesi za kinywaji hicho cha Mbulungo.

Inaarifiwa kuwa Waangola wengi hukimbilia kwa “wachawi” waliopewa mamlaka ya juu zaidi kiimani, ili kutatua mzozo au kabla ya kufanya uamuzi wa jambo fulani, licha ya kuwa vitendo hivyo hupingwa hasa na Kanisa katika koloni hili la zamani la Ureno lenye Wakatoliki wengi.

Afisa Mteule wa Manispaa ya Camacupa, Luzia Filemone alisema “zaidi ya waathiriwa 50 walilazimishwa kunywa maji haya ya ajabu ambayo, kwa mujibu wa washauri wa jadi, yanathibitisha kwamba mtu huyo anafanya uchawi au la, pia idadi ya vifo vilivyohusishwa na unywaji wa Mbulungo iliongezeka kutoka 30 hadi 50.”

Ipo hivi, imani za kishirikina zinakwamisha haki za binadamu na ni vyema kuangazia chanzo chake. ili kupata suluhu la kudumu kwani husababisha hata watu kutoendelea wakiogopa kufanya maendeleo kwa hofu ya kurogwa. Aidha, mauaji ya watu wenye Ulemavu wa Ngozi na Wazee maeneo mbalimbali, husababishwa na imani hizi za kishirikina.

Kimantiki, imani zote zinaendeleza chuki, sio ushirikina pekee kwani kila upande mmoja wa imani huona upo sahihi na ni bora kuliko wengine na hivyo hupelekea watu kuchukiana kwa kigezo cha utofauti wa kiimani, hivyo ni bora watawala wakatafuta mbinu za ziada na mbadala katika kukabiliana na mambo kama haya ili kuhakikisha kila upande unaheshimu imani ya mwingine bila kuleta madhara.

Hata hivyo, hakuna Taifa lisiloamini ushirikina, wote wameathiriwa lakini wanatofautiana viwango na namna ambavyo wanazitumia imani zao kuleta madhara katika maisha, maana hata Tanzania iliwahi kutajwa kuwa ni nchi ya pili kwa kuamini ushirikina ikitanguliwa na Cameroon kutokana na matukio yanayohusishwa na imani za kishirikina ikiwemo mauaji ya Wazee 117 katika kipindi cha Julai 2017 – Mei 2018.

‘Wachawi’ hawa wa Angola ni kama waliamua kufa kifo rahisi sana kutokana na kile ambacho walikiamini, na tabia hii inadaiwa kuwa imeenea sana kwa wao kunywa sumu ambayo inajulikana ni sumu lakini wakiwa na imani kuwa kama hawajihusishi na uchawi basi hawawezi kudhurika kitu ambacho si sahihi, Wakongo wana msemo wao wanasema “Ncha ya Kisu haipigwi kofi” …. yametokea Angola tuchukue tahadhari.

'Mti wa Uzima' wenye miaka 1,500 Limpopo
Tabora: Mwl. Doto Jela maisha kwa kubaka mtoto