Boniface Gideon, Handeni – Tanga.
Watu wanane wamefariki Dunia Wilayani Handeni Mkoani Tanga, baada ya magari mawili Lori la mizigo na Basi dogo la abiria aina ya Toyota Coaster kugongana katika Kitongoji cha Kwachuma kilichopo Kata ya Segera.
Taarifa ya Jeshi la Polisi iliyomnukuu Kamanda wa Polisi, Almachius Muchunguzi imeeleza kuwa ajari hiyo imetokea Desemba 24, 2024 majira ya saa 11:00 Alfajiri.
Amesema, Lori hilo aina ya Sharkman lenye za usajili wa T 780 DRL likiwa na Tela namba T 692 ESH mali ya Kampuni ya Starling Gulf Trading Company, likitokea Jijini Tanga kwenda Dar es Salaam, liligongana na Coaster hiyo yenye namba za Usajili T 706 DPJ, likitokea Jijini Dar es salaam kwenda Mkoani Kilimanjaro.
“Katika ajali hiyo, vifo vya watu wanane kati ya hao ni Wanaume ni watano na majeruhi wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Korogwe Magunga na Miili ya Marehemu zikihifadhiwa katika chamba cha Maiti katika hospitali hiyo,” ilieleza taarifa hiyo
Kamanda Muchunguzi amesema chanzo cha ajari hiyo ni Dereva wa Coaster kushindwa kulimudu kutokana na kutembea kwa mwendo mkali, hali iliyosababisha kutokea kwa ajali hiyo.
“Chanzo cha ajari hiyo, ni Dereva wa gari aina ya Toyota Coaster kushindwa kulimudu kutokana na kutembea kwa mwendo mkali, niwatake madereva wote kuzingatia Sheria za Barabarani, hatutasita kuchukua hatua kwa mtu yeyote atakayevunja Sheria za usalama Barabarani na tupo chonjo saa 24 hivyo atakayekiuka Sheria za usalama Barabarani tutamchukulia hatua kali za kisheria,” alisema Afande Muchunguzi