Zaidi ya wafungwa 1,500 wameripotiwa kutoroka Gerezani Nchini Msumbiji, wakitumia fursa ya machafuko yaliyochochewa na uthibitisho wenye utata wa ushindi wa Chama Tawala cha Frelimo katika uchaguzi wa hivi karibuni.
Akiongea mbele ya waandishi wa Habari, Mkuu wa Polisi wa Taifa, Bernardino Rafael alisema jumla ya wafungwa 1,534 walitoroka kutoka Gereza hilo lenye ulinzi mkali lililoko takriban kilomita 15 kutoka mji mkuu wa Maputo.
“Kati ya waliokuwa wakijaribu kutoroka, 33 waliuawa na 15 walijeruhiwa katika makabiliano na walinzi wa gereza. Operesheni ya kuwatafuta wahalifu hao, iliyosaidiwa na jeshi, ilisababisha kukamatwa kwa takriban watu 150,” alisema.
Aidha, Rafael amesema Wafungwa 30 kati ya waliotoroka walihusishwa na makundi yenye silaha ambayo yamesababisha machafuko na mashambulizi katika mkoa wa kaskazini wa Cabo Delgado, kwa miaka saba iliyopita.