Boniface Gideon, Tanga.
Kanisa la Glory Temple la Jijini Tanga, limetoa misaada wa mavazi,vyakula na vinywaji kwa makundi mbalimbali yenye mahitaji maalumu ikiwemo wazee walemavu wajane na waraibu wa dawa za kulevya ambao wanapatiwa huduma katika nyumba za upataji nafuu ‘Sober house.’
Mzee wa Kanisa hilo, Batholomayo Sigara amewaeleza Waandishi wa Habari kuwa, lengo la kutoa misaada hiyo ni kutimiza maagizo ya Yesu kupitia Amri ya kupendana.
Amesema, “tunafanya hivi kila mwaka,lengo ni kutimiza maagizo ya Yesu kupitia Amri Kuu aliyotuambia tupendane, hivyo na sisi tunaonyesha Upendo wa dhahiri kupitia kuzaliwa kwake, kwa ishara Kuu kwamba sisi wanadamu ni muhimu kupendana.”
Sigara aliongeza kuwa, Krismas ya mwaka huu wametoa Misaada wa vyakula,nguo,viatu na vinywaji kwa watu wenye mahitaji maalumu.
“Utoaji wa Msaada wa mwaka huu upo tofauti na miaka mingine,ambapo huwa tunatoa misaada mpaka ya vyerehani, ving’amuzi, tv, nguo, viatu, vyakula na vinywaji,” alifafanua Sigara.
“Kwa mwaka huu, kidogo Kuna mabadiliko, Msaada wetu ni wa vyakula, mavazi na vinywaji, Kanisa litaendelea kusaidia jamii yetu,na tunawaomba watu wengine nao wasisite kufanya hivi,ili na wenzetu waliopo kwenye makundi maalumu wajisikie furaha kusherekea sikukuu,” alisisitiza Sigara.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Asasi ya Gift of Hope inayolea waraibu wa dawa za kulevya Jijini Tanga Sober house, Said Bandawe alilishukuru Kanisa hilo kwa misaada wanayoitoa kwa jamii hiyo.
Alisema, “tunawashukuru sana,kwa misaada mnayoitoa kwetu,hawa ndugu zetu waraibu wa dawa za kulevya,wanahitaji kupata huduma nyingi sana za kijamii, kwahiyo tusiache kuwasaidia kwakuangalia hali zao zilivyo.”