Jeshi la Polisi Mkoani Kilimanjaro, limetoa taarifa ya ajali iliyotokea majira ya saa tisa na dakika arobaini jioni hii leo Desemba 26, 2024 huko kijiji cha Kibaoni Tarafa ya Tarakea Wilaya ya Rombo Mkoa wa Kilimanjaro barabara kuu ya Moshi -Tarakea.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa, gari lenye namba za usajili T. 620 DZQ Bus Yutong kampuni ya Ngasere ikitokea Dodoma kwenda Tarakea iligongana na gari dogo la abiria lenye namba za usajili T959 CKU Toyota Noah.
Noah hiyo ilikuwa ikitokea Tarakea kwenda Moshi na ajali hiyo imesababisha vifo vya watu tisa ambao wote walikuwa kwenye gari namba T959 CKU Toyota Noah.
“Waliofariki katika ajali hiyo na kufahamika ni Mamasita Lowasa (27), mkazi wa Kamwanga, Damarisi Kanini Mwikau, (22), mkazi wa Elast Kenya, Peter Alex Urio (38), 4. Monica Joyce Mumbua (64) Mkenya.
Wengine ni Eligatanasi Kanje (30), mkazi wa Tarakea na Hilda Francis Leberatus, (24), mkazi wa Kikelelwa huku Miili mingine ya watu watatu ikiwa haijatambuliwa.
Aidha taarifa hiyo imebainisha kuwa pia kuna Majeruhiwa mmoja aliyekuwa mtembea kwa miguu ambaye majina yake hayajafahamika na amepelekwa Hospitali ya Huruma Wilaya ya Rombo kwa matibabu.
“Uchunguzi wa awali umebaini chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa Dereva wa gari dogo la abiria Noah kuyapita magari mengine bila kuchukua tahadhari,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Miili ya marehemu imehifadhiwa hospitali ya Huruma Wilaya ya Rombo kusubiri uchunguzi na taratibu zingine.