Ligi kuu Uingereza imeendelea kuwa gumzo wakati huu wa Skukuu za Krismasi baada ya vigogo kadhaa kufanya vibaya kwenye michezo yao na baadhi ya timu ambazo hazikuimbwa mwanzoni mwa ligi kugeuka kuwa tishio kwa kila mpinzani wanayekutana naye. Hizi ni baadhi ya mechi ambazo zimekuwa gumzo nyakati hizi.

Chelsea yapoteza kwa  Nyumbani

Fulham imewashangaza mashabiki wa soka baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 nyumbani kwa Chelsea. Sote tumeishuhudia Chelsea ikirejesha makali yake kwa siku za hivi karibuni baada ya kujikusanyia alama 13 katika mechi 5 na kugeuka washindani wa Liverpool.

Katika mchezo huo Chelsea walikuwa wa kwanza kupata bao la uongozi kupitia kwa Cole Palmer dakika ya 16.Mpaka dakika ya 81 Chelsea walikwishajihakikishia kuondoka na alama tatu lakini mambo yalibadilika baada ya Harry Wilson kufunga bao la kusawazisha dakika ya 82 na Rodrigo Muniz kufunga bao la pili dakika ya 90+5.

Kupoteza dhidi ya Fulham kunawafanya watofautiane alama 7 na Liverpool aliye na mchezo mmoja mkononi.

Manchester United mambo bado magumu

Tangu mwezi Disemba umeanza Manchester United imeshinda mchezo mmoja pekee dhidi ya Manchester City. Timu hiyo chini ya Ruben Amorim imekuwa na wakati mbaya zaidi baada ya kufungwa na Wolves siku ya Boxing Day. Mpaka sasa United imepoteza michezo 8 kushinda 6 na sare 4 ikiwa na alama 22 pekee na kushika nafasi ya 14 kwenye msimamo wa ligi ya Uingereza.

Amorim amekuwa na wakati mbaya tangu atue United na siku chache zilizopita aliondoshwa kwenye michuano ya EFL baada ya kipigo cha mabao 4-3 kutoka kwa Totenham. Kwa sasa United imepoteza mvuto kwa mashabiki wake na hata thamani yake imeporomoka sokoni.

Manchester City ya Guardiola ni pasua kichwa

Kama kuna makocha wana wakati mgumu basi ni Pep Guardiola, Tangu mwezi Novemba uanze Manchester City imekuwa na wakati mbaya zaidi kwa miaka 10 iliyopita. Sare ya bao 1-1 dhidi ya Everton imewafanya City kukusanya alama 4 pekee katika michezo 5 ya EPL waliyocheza hivi karibuni.

Manchester City imepoteza michezo 6 kati ya 18 waliyocheza mpaka sasa,wakishinda michezo 8 na sare 4. Wanakwenda kumaliza raundi ya kwanza ya EPL dhidi ya Leicester City Disemba 29 kama watashinda mchezo huo watafikisha alama 31 na itakuwa ni mara yao ya kwanza kumaliza mzunguko wa kwanza wakiwa na alama chache kwa misimu ya hivi karibuni.

Nottingham wanaiwinda Top Four kimya kimya

Ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Tottenham unawafanya Nottingham kuwa na mwenendo mzuri wa mechi tano zilizopita. Timu hiyo imeshinda mechi 4 mfululizo wakijikusanyia alama 12 katika michezo 5 ya karibuni.Timu hiyo imeshinda mechi 10 sare 4 na kupoteza 4 wakijikusanyia alama 34.

Nottingham United ni moja ya timu tatu zilizofungwa mabao machache kwenye msimamo wa ligi.Timu hiyo imefungwa mabao 19 pekee .Arsenal imefungwa mabao 16 na Liverpool imefungwa mabao 17. Kama timu hii itakaza buti na kuongeza nguvu kwenye safu ya ushambuliaji basi tutegemee kuiona ikishiriki Uefa msimu ujao na kurudia historia yake ya miaka ya 80.

Viongozi mna wajibu wa kuhubiri amani - Dkt. Mwinyi
Mohammed Salah aweka rekodi mpya Liverpool ikijenga kiota kileleni