Imeelezwa kuwa Tanzania haikuchaguliwa kwa bahati mbaya kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati, isipokuwa imekidhi vigezo ambavyo waandaji wamejiridhisha navyo.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Noel Kaganda alipokuwa anatoa mada katika semina maalum kwa waandishi wa habari kuhusu uenyeji wa Mkutano huo.
Semina hiyo inayofanyika kwenye Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam Januari 5, 2025 imefunguliwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa ambaye aliwaomba waandishi wa habari kutumia vizuri kalamu na sauti zao kutangaza mkutano huo na fursa zake kwa wananchi.
Balozi Kaganda alizitaja sababu hizo kuwa ni pamoja na Tanzania kuwa ni moja ya nchi chache za Afrika zenye mipango thabiti ya kuwa na nishati ya kutosha na uhakika, mpango wa kusambaza umeme nchi nzima ikiwa ni pamoja na vijiji na vitongoji.
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa kinara wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, mikakati kabambe ya upatikanaji wa nishati ambapo malengo ifikapo 2030 asilimia 75 ya Watanzania wawe wamefikiwa na umeme na asilimia 80 wawe wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034
Sababu nyingine alizozitaji kuwa ni kuimarika kwa diplomasia ya Tanzania, amani na usalama na uzoefu wa kutosha wa kuwa nwenyeji wa mikutano mikubwa ambayo imekuwa ikifanyika nchini.
Mkutano huo unaondaliwa kwa ushirikiano baina ya Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika, Kamisheni ya Umoja wa Afrika na Tanzania unalenga kuwakutanisha wakuu wa nchi zote za Afrika na wadau wengine ili kujadili kwa pamoja njia za kuchagiza upatikanaji wa nishati ya uhakika na nafuu kwa kutumia rasilimali zilizopo.
Mkutano huo utakaofanyika jijini Dar Es Salaam Januari 27 na 28, 2025 utahitimishwa kwa nchi 14 kusaini Mpango wa Nishati ambao ni ahadi ya Serikali zao kuchukua hatua mbalimbali za kufikisha umeme kwa wananchi.
Nchi hizo ni Tanzania, Liberia, Senegal, Niger, Nigeria, Chad, Mauritania, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Côte d’Ivoire, Burkina Faso, Malawi, Msumbiji na Zambia.
Mkutano huu unaojulikana kwa kifupi kama Mission300 utajiwekea malengo ya kuwafikishia umeme watu milioni 300 kati ya watu milioni 685 wanaoishi bila umeme barani Afrika, ifikapo mwaka 2030.