Watu watano, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma na kusomewa mashtaka ya uhujumu uchumi, kutokana na tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi.
Wakisomewa mashtaka hayo Mawakili Waandamizi wa Serikali, Patricia Mkina na Zubeda Lyaumi wamesema Desemba 24, 2024, washitakiwa walikamatwa katika eneo la stendi kuu ya mabasi Nanenane, mkoani Dodoma, wakiwa na magunia 15.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Denis Mpelembwa, amewataka watuhumiwa hao kutokueleza chochote kutokana na mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo la uhujumu uchumi,Huku kesi hiyo ikiwa haina dhamana na watuhumiwa wataendelea kusalia mahabusu kutokana na Kesi hiyo kuahirishwa hadi Januari 20, 2025.
Watuhumiwa hao ni Theddy David, Fidelis Marwa, Emmanuel Mwamlaga, Shabani Rashidi na Anna Bosco ambaye ni Kondakta wa basi, waliokamatwa wakiwa na magunia 15 ya bangi yenye uzito wa kilo 300.88 katika basi lenye namba za usajili T882 EDS, walilokuwa wakisafiria kutoka mkoani Mara kwenda Dar es Salaam.