Kufuatia mafanikio katika uimarishaji wa mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya mkoani Kagera unaotekelezwa na Bohari ya Dawa – MSD, ambao umepunguza malalamiko ya upungufu wa bidhaa za afya, Katibu Tawala wa Mkoa huo, Stephen Ndaki amewapa kongole.
Ndaki alitoa pongezi hizo wakati akizungumza na ujumbe maalum kutoka MSD, ukiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya MSD, Rosemary Silaa ikiwa ni ziara maalum ya kuadhimisha miaka 30 ya MSD walipomtembelea ofisini kwake.
Amesema, maboresho ya huduma za MSD yamesaidia kuondoa kero na malalamiko ya mara kwa mara yaliyokuwepo miongoni mwa jamii na wateja juu ya uhaba wa Dawa vituoni, hivyo kupelekea kuimarika kwa hali utoaji wa huduma za afya Mkoani humo.
Ndaki aliongeza kuwa, mbali na kuimarika kwa utoaji huduma, hivi sasa uelewa wa majukumu ya MSD na jinsi inavyofanya kazi zake, umeongezeka miongoni mwa viongozi hivyo kuondoa kasumba ya kutupiana lawama juu ya ununuzi ya bidhaa za afya, baina ya MSD na Wateja wake, kwani viongozi wote ndani ya Mkoa huo wamejengewa uelewa.
“Hapo mwanzo kulikuwa na kelele sana kutoka vituoni kwamba tumelipa lakini MSD hajaleta, hatahivyo kwa siku za hivi karibuni malalamiko hayo yemeondoka, na uelewa juu ya mnyororo wa bidhaa za afya umeongezeka mpaka kwa viongozi, hivyo tuwapongeze kwa maboresho,” alibainisha.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya MSD, Rosemary Silaa alieleza ni jinsi gani MSD ilivyopitia katika vipindi tofauti, na jinsi ilivyojizatiti kuboresha huduma zake, ili kupunguza, ama kuondoa kabisa changamoto chache zilizoukabili mnyororo wa bidhaa za afya.
Alisema, MSD imeendelea kuboresha mikataba yake na wazalishaji na washitiri, kuajiri kada mbalimbali Ili kukidhi mahitaji ya huduma za MSD kwa wateja, kuboresha na kuimarisha mifumo ya kiutendaji, kuboresha huduma na mawasiliano na wateja wake, Ili kuhakikisha inatatua changamoto chache zilizobakia katika upatikanaji wa bidhaa za afya nchini.

AC Milan yafanya ubaya Ubwela kombe la Supercoppa Italy
Carragher afichua kilichopelekea Liverpool kupata sare