Paris St-Germain wana nia ya kumsajili Jhon Duran na inaaminika Aston Villa wanaweza kushawishika kumuuza mshambuliaji huyo wa Colombia mwenye umri wa miaka 21 kwa £60m. (Sportsport)
Mkurugenzi wa michezo wa Barcelona Deco amekutana na wawakilishi wa Duran kwa mazungumzo yasiyo rasmi ili kumjulisha mshambuliaji huyo wa Aston Villa kuwa yuko kwenye rada za klabu hiyo ya Catalan. (Sport – kwa Kihispania)
Bayern Munich wanataka kuvuruga ombi la Manchester United la kutaka kumsajili mshambuliaji wa Uswidi Viktor Gyokeres, 26, kutoka Sporting. (Star)
Real Madrid wamekataa nafasi ya kumsajili mlinzi wa Uholanzi Virgil van Dijk, 33, ambaye atakuwa mchezaji huru mkataba wake wa Liverpool utakapokamilika msimu wa joto. (Relevo – kwa Kihispania)
Ligi ya Saudia ina matumaini ya kumsajili kiungo wa kati wa Brazil Casemiro, 32, kutoka Manchester United mwezi huu. (Telegraph – usajili unahitajika)
Manchester United na Tottenham wanatathmini uwezekano wa kumsaini mshambuliaji wa Ufaransa Randal Kolo Muani kwa mkopo kutoka Paris St-Germain, huku Juventus pia ikimtaka mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26. (Athletic – usajili unahitajika)
Marcus Rashford, 27, anasakwa kwa mkopo na AC Milan lakini mkataba wowote utategemea Manchester United kulipa sehemu kubwa ya mshahara wa mshambuliaji huyo wa Uingereza. (Guardian)
Juventus wana nia ya kumsajili mshambuliaji wa Uholanzi Joshua Zirkzee kwa mkopo lakini mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23 hana nia ya kuondoka Manchester United. (Sky Sports)
Manchester United wamepewa ofa ya kumsajili mshambuliaji wa Juventus na Serbia Dusan Vlahovic mwenye umri wa miaka 24 katika mkataba wa kubadilishana na Zirkzee. (Team Talk)
Real Betis ni miongoni mwa vilabu kadhaa vinavyotarajia kumsaini winga wa Manchester United wa Brazil Antony, 24, kwa mkopo kwa msimu uliosalia. (Independent)
Antony pia anahusishwa kwa mkataba wa mkopo na klabu ya Ugiriki ya Olympiakos. (Sun)
Mshambuliaji wa West Ham Niclas Fullkrug pia ananyatiwa na Juventus, huku klabu hiyo ya Italia ikitaka kumsajili kwa mkopo mchezaji huyo wa kimataifa wa Ujerumani mwenye umri wa miaka 31. (Calciomercato – kwa Kiitaliano)
Mshambulizi wa Brazil Matheus Cunha, 25, bado hajafanya uamuzi iwapo atasaini mkataba mpya na Wolves au la. (Sky Sports)
Chelsea wanajadili iwapo watasitisha mkataba wa mkopo wa beki Muingereza Trevoh Chalobah, 25, katika klabu ya Crystal Palace au kumsajili beki mpya mwezi huu. (Team Talk)
Liverpool wanajiandaa kumnunua winga wa Feyenoord wa Algeria Anis Hadj Moussa, 22. (Football Insider)