Baada ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda kudai mbele ya Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega kwamba Mbunge wa jimbo la Arusha Mjini, Mrisho Gambo haudhurii vikao kama inavyotakiwa, jipya limeibuka.
Gambo akiongea hii leo Januari 7, 2025 mjini Arusha amemjibu Makonda kwa kusema yeye si Mfanyakazi wa Serikali, bali ni Mwakilishi wa Wananchi na Mtu anayeweza kutoa taarifa na rekodi kwamba hahudhurii vikao kwa mujibu wa sheria ni Bunge la Tanzania.
Amesema, “lazima afahamu kwamba mimi sio Mfanyakazi wa Serikali, mimi ni Mwakilishi wa Wananchi, mimi ni Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mtu ambaye anaweza kutoa taarifa na rekodi kwamba sihudhurii vikao kwa mujibu wa sheria ni Bunge na sidhani kama yeye kwa nafasi yake ni sehemu ya Bunge.”
Hata hivyo Mbunge Gambo ametolea ufafanuzi sula hilo akidai kuwa ile ilikuwa ni ziara ya Waziri wa Ujenzi na kwamba aliyemuuliza ni Waziri wa Ujenzi na alitegemea ndiye angeweza kumpatia majibu ya changamoto zinazowakabili na si Makonda kama alivyofanya.
“Ule mkutano haukuwa mkutano wa Mkuu wa Mkoa, ile ziara haikuwa ziara ya Mkuu wa Mkoa, ilikuwa ni ziara ya Waziri wa Ujenzi na mimi niliyemuuliza ni Waziri wa Ujenzi nilitegemea yeye ndiye angeweza kutupatia majibu ya changamoto yetu lakini cha kushangaza zaidi nikaona Bwana Makonda ametoa majibu ambayo kimsingi hayakuhusiana na hoja ambazo nimezijenga,” alisema Gambo.