Jamii Nchini, imehimizana kuchukua tahadhari na hatua stahiki za kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza, ikiwemo kubadili mwenendo wa ulaji usiofaa, kutokana na magonjwa hayo kuchangia vifo vingi ulimwenguni.

Wito huo umetolewa kwa nyakati tofauti na Wakazi wa maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam wakati wakihojiwa na Dar24 Media juu ya suala la uzingatiaji wa masuala ya afya na mazoezi, ili kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza na kuuitaka jamii kula mboga mboga na matunda.

Saulo Kaseya, ambaye ni Mkazi wa Mbezi yeye alisema pia kila mtu ana wajibu wa kudhibiti matumizi ya vilevi kama sigara na pombe na kutoa hamasa kwa jamii pia shughuli za nguvu na kuzingatia mlo unaofaa hasa kwa kuondoa au kupunguza viungo vya chumvi, sukari na mafuta.

“Tunaelimishwa kila siku, Magonjwa yasiyoambukizwa yanakua tishio kwa afya zetu, sasa tujipange kukabiliana nayo maana yana madhara makubwa ingawa kuna uwezekano wa kuyadhibiti, tupunguze ulaji usiofaa na tuongeze bidii ya kula vyakula vya mboga mboga na matunda,” alisema.

Naye Mariam Abdallah kwa upande wake aliongeza kuwa jamii pia inatakiwa kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi angalau dakika 30 mara tatu kwa wiki na kwamba inapasa kukabiliana na magonjwa mengine kama inavyoelekezwa na wataalam.

Alisema, “tuendelee kuhamasishana hata kuanzisha na kujiunga kwenye vikundi vya mazoezi ya pamoja kwani vikundi hivi husaidia sana kuleta hamasa ya kufanya mazoezi, tutumie fursa hizo kwa kushirikisha vikundi vya mazoezi vilivyopo kwenye kata, mitaa au vijiji.”

MAKALA: Huba la Kondoo kwa Mbwa shujaa
Usililojua: Binadamu huzaliwa na mkia