Baadhi ya Wananchi katika Kijiji cha Chamae kilichopo Wilayani Kongwa Mkoani Dodoma, wamehimizana kuendelea kutoa tahadhari kwa kila kaya, kuhifadhi chakula kidogo walicho nacho na kutokukitumia kwa ajili ya kutengenezea pombe za kienyeji kutokana na changamoto za hali ya hewa ambayo wanahofu huenda ikaathiri msimu wa mavuno.
Wakiongea kwa msisitizo, Wananchi hao akiwemo Vicent Chisatu amesema wengi wa Wanakijiji huenda hawana ufahamu na masuala ya hali ya hewa jinsi yanavyoweza kuathiri upataji wa mazao wakati wa kipindi cha mavuno, huku wakitumia akiba waliyonayo kuuza ama kutengenezea Pombe, ili kupata pesa za kujikimu.
Amesema, “Nchi mzima tunachangamoto ya mvua, kumekuwa na ukame hivyo kwamimi wito wangu kila mmoja asichoke kumwambia mwenzie ahifadhi chakula alichopata msimu huu, tutumie vizuri akiba hiyo na tuhifadhi chakula tusipikie pombe na tusiuze hali ya hewa haitabiriki tutakao umia ni sisi.”
Kwa upande wake Meshaki Mtangoo alisema jamii itakakiwa kuondoa dhana ya msaada wa Serikali ambayo imekuwa ikihakikisha inawasaidia wananchi walioathirika na ukame huku akiwataka wafugaji kuuza sehemu ya mifugo yao kwa ajili kupata fedha za kununulia chakula na kuweka akiba mapema.
“Tusikariri, akiba haiozi jamani tubadilike hivi kila mwaka tunaelemishwa hata wakisema hatuelewi ni kweli? fimbo ya mbali haiuwi nyoka kidogo ulichonacho kina faida kuliko kingi cha mbali, sasa hivi kila mtaa ukipita kuna Pombe na zote ni za nafaka hili hapana ndugu zangu,” alisisitiza Mtangoo.
Shughuli kuu za kiuchumu zinazofanywa na wakazi wa Wilaya ya Kongwa ni ufugaji wa Wanyama na Kilimo cha mazao ya chakula na biashara huku Wenyeji wake wakiwa ni Wagogo, Wakaguru na Warangi ingawa kuna makabila mengine ambayo yalihamia toka sehemu mbambali kama vile Wabena, Wanguu, Wakamba na Wamasai.