Mahakama Kuu ya Kenya, imesema Inspekta Jenerali wa Polisi, Douglas Kanja atawajibika binafsi kwa ukiukaji wowote wa haki za waandamanaji baada ya kupelekea Watu 60 kuuawa wakati wa maandamano ya Juni-Julai 2024, huku kukiwa na wasiwasi kuhusu matumizi ya nguvu kupita kiasi na vyombo vya usalama dhidi ya mikusanyiko ya amani.
Vyombo vya Habari Nchini humo vimeripoti kuwa, Makundi ya kutetea haki za binadamu hapo awali yaliilaumu polisi kwa kutumia nguvu kupita kiasi wakati wa kukabiliana na maandamano, ambapo watu waliuawa na mamia kujeruhiwa mikono ya vyombo vya usalama, wakati wa maandamano yaliyoongozwa na vijana kupinga kodi na utawala mbaya.
Uamuzi huo wa Mahakama ulitokana na kesi iliyowasilishwa na Chama cha Madaktari na Madaktari wa Meno wa Kenya (KMPDU), baada ya katibu mkuu wake, Davji Attelah kujeruhiwa na kopo la gesi ya machozi wakati wa maandamano ya Machi 2024 walipokuwa wakidai mazingira bora ya kazi.
Jaji wa Mahakama Kuu, Jairus Ngaah alisema Kanja atawajibika kwa vitendo au kutotenda ipasavyo majukumu yake kwa maafisa walio chini ya amri yake na atawajibika binafsi kwa ukiukaji wowote wa haki za waandamanaji, kwa kushindwa kuchunguza na kuwachukulia hatua maafisa wanaotumia nguvu kinyume cha sheria kuvunja maandamano.