Kufuatia Kituo cha Huduma kwa Wateja cha Shirika la Umeme Nchini – TANESCO, kushindwa kuwahudumia Wananchi kwa viwango vinavyotarajiwa, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko ameagiza kifumuliwe.
Agizo la Dkt. Biteko amelitoa hii leo Januari 9, 2025 jijini Dar es Salaam baada ya kukitembelea akilenga kufuatilia utekelezaji wa maelekezo yake aliyoyatoa Aprili, 2024.
Akiwa kituoni hapo, ameshangazwa na hatua ya TANESCO kuweka kando maelekezo ya mwezi Aprili 2024 yaliyolitaka Shirika hilo kuondokana na matumizi ya namba za kulipia kwenye utoaji wa huduma na kuomba namba ya bure ya huduma (free toll number) kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania -TCRA, ili kuwapa unafuu wananchi wanaohitaji huduma.
Amesema, “wewe ulishapiga simu, pesa yako ikakatwa na huduma usiipate? Wananchi wanaumia sana!” naagiza kuundwa upya kituo ili kuongeza ufanisi na tija kwa Wananchi, “kituo hiki kinategemewa na Watanzania wengi na huduma inayotolewa hapa hairidhishi kabisa.”
Ameongeza kuwa, Serikali imetoa fedha nyingi kuhudumia kituo hicho lakini utendaji wake ni mbovu kuliko huduma ya kituo na kutoa wiki moja kwa uongozi wa TANESCO kufanya maboresho ya Kituo hicho na matokeo yake yawe wazi kwa Wananchi kutokana na huduma zake.
TANESCO ilielekezwa kuachana na matumizi ya namba za kulipia Kwenye utoaji wa huduma na kuomba namba ya bure ya huduma (toll number) kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania-TCRA ili kuwapa unafuu wa Wananchi wanapopiga kuhitaji huduma za TANESCO.
Awali, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Mha. Abubakar Issa alisema kulikuwa na changamoto za kibajeti na kudai kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania – TCRA, watakaa haraka na kuanza matumizi ya namba bila malipo, ili kutoa unafuu kwa Wananchi.