Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa amezindua Mikakati sita ya Mawasiliano ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Vyombo vya Usalama na kuagiza utekelezaji wa mikakati hiyo kuanza ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi kwa kuhabarisha na kushirikisha umma kwenye utekelezaji wa majukumu.

Bashungwa amezindua mikakati hiyo leo tarehe 09 Januari 2025 jijini Dodoma ambapo hafla hiyo imeambatana na ufungua Kikao Kazi cha Mwaka cha Wasemaji wa Vyombo vya Usalama pamoja na Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

“Kuandaliwa kwa mikakati ni hatua kubwa kwa Wizara na Vyombo vyake vya Usalama, niwasihi Wakuu wote wa Vyombo vya Usalama, kuhakikisha mikakati hii inaanza kutekelezwa kuanzia sasa ili kutimiza lengo letu la kuongeza ufanisi wa kiutendaji katika kuhabarisha na kushirikisha Umma wa Watanzania kwenye kutekeleza majukumu yetu” amesisitiza Bashungwa.

Bashungwa ameelekeza Vyombo vya Usalama kutenga bajeti ya utekelezaji wa mikakati ya mawasiliano kwa kuwa ina tija katika kuleta mabadiliko chanya kwenye kuhudumia na kuhabarisha wananchi kwa kuongeza uelewa, na ushiriki wa jamii katika masuala ya usalama wa raia na mali zao pamoja na utunzaji wa amani na utulivu wa nchi.

Aidha, Bashungwa amewaka Wasemaji wa Vyombo vya Usalama na Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano wa Wizara kufanya tathmini ya pamoja kuhusu utendaji kazi wa vitengo vya Habari, Mawasiliano, na Uhusiano pamoja na kuwajengea uwezo Maafisa Habari katika kutumia teknolojia za kisasa za mawasiliano.

Kadhalika, Bashungwa rai kwa wananchi kujipanga kupokea ugeni wa Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika utahusisha Wakuu wa Nchi 54 kutoka Bara la Afrika unaotarajiwa kufanyika tarehe 27 na 28 Januari, 2025 Jijini Dar es Salaam na amewasisitiza kutumia kikamilifu fursa mbalimbali zitakazopatikana.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo ameeleza kuwa mikakati ya mawasiliano ndio nyenzo muhimu ya kufanikisha azma ya kufikisha taarifa kwa umma kuhusu utekelezaji wa majukumu na program mbalimbali za Wizara na Vyombo vya Usalama na kusisitiza utekelezaji wake kusimamiwa ipasavyo.

Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ally Gugu ameeleza kuwa mikakati ya mawasiliano imeandaliwa kwa lengo la kutekeleza Maelekezo ya Serikali ya kuimarisha shughuli za habari na Mawasiliano, ili kuiwezesha jamii kupata taarifa kwa wakati, kwa kutumia teknolojia za kisasa hivyo kuifikia jamii kwa wakati ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai.

Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali ikiwa ni pamoja Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Maduhu Kazi na Wakuu wa Vyombo vya Usalama ambavyo ni Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Idara ya Uhamiaji pamoja na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).

Habari kuu katika Magazeti ya leo Janauri 10, 2025
Dkt. Biteko aishangaa TANESCO, agiza kituo kifumuliwe