Ziara ya Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Daniel Sillo ya kutembelea kituo cha uchakataji wa taarifa za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa – NIDA, imeibua mapya baada ya Mkurugenzi Mkuu wake, James Kaji kudai kuwa watu 600,000 wamebainika kufanya udanganyifu wa majina bandia.
Kaji ameyasema hayo hii leo Januari 10, 2025 jijini Dar es Salaam, ikiwa zimepita siku 25 tangu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa kutoa siku 60 kwa NIDA kuhakikisha inasambaza vitambulisho Milioni 1.2 vilivyo tayari.
Amesema, “wapo waliosoma kwa majina tofauti na wanayo tumia sasa, na wale walioachishwa kazi kwa kutumia majina feki na sasa wanatamani kutumia majina yao halisi changamoto iliyopo ni kuwa alama za vidole zinasoma jina alilotumia mwanzo na hivyo kuongeza idadi ya majina feki.”
Aidha, Kaji amesema kutumia kwa mfumo mpya wa kutuma ujumbe mfupi kwa wale ambao vitambulisho vyao viko tayari umefanya kuwafikia watu 400,000 ndani ya wilaya 87 kati ya wilaya 153 hadi kufikia Januari 8, 2025.
Akiwa katika ziara hiyo, Naibu Waziri Sillo amesema ameridhishwa na utendaji kazi wa NIDA akidai uzalishaji wa namba na vitambulisho unafanyika kwa kasi huku akiwataka Watanzania kufuata vitambulisho vyao mara watakapopokea ujumbe kwenye simu zao za viganjani.