Johansen Buberwa – Kagera.
Baadhi ya wavuvi wanaofanya shughuli zao katika mwalo wa Igabiro na Lukoijo katika Kata ya Kaagya Wilayani Bukoba Mkoani Kageram wameiomba Serikali kuwasaidia kujenga mahusiano ya ujirani mwema na Wavuvi wa nchi ya Uganda ikiwemo kuwawekea mipaka ndani ya ziwa Victoria na kuangalia upya sheria za uvuzi za pande zote mbili, ili iwasaidie kujikwamua kiuchumi.
Ombi hilo limetolewa wakati na Wavuvi hao wakati wa ziara ya Mkuu wa Wilaya Bukoba, Erasto Sima katika maeneo hayo ambapo walitumia fursa hiyo kuelezea adha wanazozipa wakati wakitekeleza majukumu yao kwenye ziwa Victoria, wakisema sheria za uvuvi zinazofanana pamoja na kuimarisha doria kwa nchi ya Tanzania ndani ya ziwa hilo italeta mahusiano mema na kuepuka kukamatwa na Polisi wa Uganda.
Wamesema, “shughuli zetu za uvuvi zinakumbwa na changamoto za sintofahamu kwa jeshi la Uganda ambalo linakamata tu katika maeneo yetu tunapofanyia shughuli zetu za uvuvi ni eneo la Uganda hadi Bukoba mjini na kerebe wanasema ni mali yao wanasema sisi tunatakiwa kufanyia shughuli zetu kwenye eneo la mwanza na kuendelea kwa maelezo yao hatutakiwi kuvua katika ziwa hili.”
William Mchome katika BMU Lukoijo, kwa upande wake alidai kuwa, “sisi tunatambua eneo hilo ni sehemu ya nchi yetu ya Tanzania, wanapokamata huwanyang’anya wavuvi wetu simu zao na kuwatishia kuwapiga risasi kisha kuwapeleka kwenye kambi yao na kuamuru kupiga simu kwa wamiliki na kutaka kiasi cha shilingi milioni moja na nusu na kuendelea kwa malipo ambayo hayana risiti na kudai kutaifisha baadhi ya vifaa ikwemo taa na betri.”
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kaagya, Stanley Ngaiza amesema kuna umuhimu wa Askari Maji wa nchi zote mbili kuwa na mahusiano ya ujirani mwema, wakati Serikali ikiwa inatafuta utaratibu mwingine hali itakayo saidia kuweka mahusiano mazuri.
Akijibu hoja hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Erasto Sima amesema Serikali imelipokea jambo hilo na litafanyiwa kazi kwa kulitatua na kuwataka wavuvi hao kuwa na ushirikiano.