Kwa mujibu wa Kamusi elezo, Wingu ni matone madogo ya maji yanayoelea pamoja katika angahewa juu ya ardhi, aidha tafsiri nyingine inadai kuwa Mawingu ni mahali ambako mvua na theluji hutoka.
AINA ZA MAWINGU.
Zipo aina nyingi za mawingu na majina yake yanatokana na umbile, kimo au tabia zake, huku ikiekezwa kuwa yana athari kubwa katika usafiri wa anga, hivyo huwezi kutenganisha hali ya hewa na usafiri wa anga.
i. CIRRUS – Haya yametengenezwa na chenga za barafu na huonekana kama mitiririko mirefu, nyembamba, na nyeupe angani, huku Wataalamu wakisema ukiona haya basi hali ya hewa iko poa.
ii. CirroCUMULUS – Ni mfano wa pamba ndogo zenye mviringo ambazo kawaida huonekana katika kimo kirefu juu angani, kwa kawaida huwa ni meupe, lakini wakati mwingine huonekana kijivu na hutokea kipindi cha hali ya hewa nzuri lakini yenye baridi.
iii. CirroSTRATUS – Haya ni mawingu mfano wa karatasi nyembamba ambayo kawaida hufunika anga lote.
Mawingu ni nyembamba sana kiasi kwamba Jua au mwezi wakati mwingine zinaweza kupenyeza mng’ao na kuonekana kwa mbali na kwa kawaida huja masaa 12 hadi 24 kabla ya mvua au dhoruba ya theluji.
iv. AltoCUMULUS – Hili ni wingu la kiwango cha katikati, likiwa na mabaka ya kijivu-nyeupe na baadhi ya sehemu nyeusi kuliko nyingine, ambapo kwa kawaida hukaa makundi makundi karibu kilomita moja ya unene na ukiona mawingu ya altocumulus kwa asubuhi yenye joto na baridi, kunaweza kuwa na mvua ya ngurumo alasiri.
v. AltoSTRATUS – Ni mawingu ya kiwango cha katikati, kijivu ambayo kawaida hufunika anga lote na Jua au mwezi huweza kuangaza kupitia wingu la altostratus, lakini itaonekana ukungu, unaambiwa ukiona mawingu ya altostratus basi dhoruba au mvua inayoendelea au theluji inaweza kuwa njiani.
Mara nyingi mvua huanza kujiunda katika wingu hili, na ikiwa mvua itaendelea basi wingu linageuka la mvua nimbostratus.
vi. STRATUS – Haya ni ya chini na yana rangi ya rangi ya nyeupe kijivu na inaweza kufunika baadhi ya anga yote. Mawingu ya Stratus yanaweza kuonekana kama ukungu ambao haufiki chini, yenye ukungu mwepesi au manyunyu wakati mwingine huanguka.
vii. StratoCUMULUS – Haya nayo ni Mawingu ya chini yenye uvimbe na kijivu na wakati mwingine hujipanga kwa safu au kuenea, lakini ili kutofautisha kati ya stratocumulus na wingu la altocumulus, elekeza mkono wako kuelekea kwenye wingu. Ikiwa wingu lina ukubwa wa ngumi yako, basi ni stratocumulus.
viii. CUMULUS – Mawingu haya yana ukuaji wa wima, ni mawingu yenye rangi nyeupe na wepesi ambayo yanaonekana kama mipira ya pamba inayoelea ambayo huwa yanakuokoa muda mwingine jua linapokuwa kali kwa kukuletea kivuli cha muda na yanaweza kuhusishwa na hali ya hewa shwari au dhoruba.
ix. NIMBOSTRATUS – Ni wingu la mvua kijivu, giza na hukaa chini angani, yanayohusishwa na mvua inayoendelea au theluji, ila wakati mwingine hufunika anga lote na huwezi kuona kingo za wingu.
x. CUMULONIMBUS – Hili ndiyo wingu korofi, kiboko ya wanaanga na wasio wanaanga, yenyewe yana ukuaji wa haraka na wima na inaweza kukua hadi kilomita 10 juu.
Sasa katika urefu huo, upepo mkali utajiunda juu ya wingu na ieleweke kwamba ni mawingu ya dhoruba na yanahusishwa na mvua nzito, theluji, mvua ya mawe, umeme, na wakati mwingine kimbunga.
Wana anga wanasema kuwa, kwa baadhi ya nyakati Ndege inapopita katika wingu hilo na ikatoka upande wa pili basi itaonekana kama imepondwa pondwa na nyundo.
credit@ucar